CCM NAKO KWAFUKA MOSHI, NAPE APIGWA KOMBORA.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amejibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ni mmoja wa mawaziri walioshindwa kazi, hivyo kustahili kung’olewa. Katika madai yake, Nape alisema Dk Kawambwa ameshindwa kusimamia vyema madai ya walimu na kwamba akiwa Waziri wa Miundombinu, aliingia mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kujenga Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga. Nape alikaririwa akisema kwamba umefika wakati kwa waziri huyo na wenzake wa Fedha, Dk William Mgimwa; Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; na Naibu wake, Adam Malima kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho. Akijibu madai hayo Mjini Bagamoyo jana, Dk Kawambwa alisema anasubiri kwa hamu kuitwa CC kueleza tuhuma zinazomkabili huku akijigamba kuwa yeye ni mti wenye matunda ndiyo maana unapigwa mawe.