Ruka hadi kwenye maudhui makuu

YANGA KUINGIA KAMBINI KUIWINDA SIMBA

Kikosi  cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, kitaingia kambini Novemba 25 kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo na mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Simba utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 14, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, Kocha wa timu yao, Mholanzi Ernie Brandts aliyeondoka nchini mara tu baada ya raundi ya kwanza ya ligi hiyo kumalizika Novemba 7, mwaka huu, atarejea nchini Jumapili Novemba 24 tayari kuanza mazoezi na wachezaji wake Jumatatu ya Novemba 25.

Simba na Yanga zitamenyana katika mchezo maalum wa Ngao ya Hisani ulioandaliwa na wadhamini wa klabu hizo kongwe nchini, Kampuni ya Bia nchini (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro ambao watatoa zawadi ya Sh. milioni 100 ambazo zimekuwa zikishindaniwa na masjhabiki wa klabu hizo kwa kunywa bia na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu (SMS).

Kizuguto alisema mara baada ya mchezo huo, kikosi hicho kitaendelea na maandalizi kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa, lakini pia timu inategemea kushiriki katika mashidano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mapema Januari mwakani.

Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ikiongoza msimamo baada ya kukusanya pointi 28, moja mbele ya Azam FC na Mbeya City wanaokamatana nafasi ya pili na tatu. Azam inashika nafasi ya pili kutokana na kubebwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, Simba ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 24.


Baada ya kuinyuka Oljoro JKT 3-0 katika mchezo wao wa mwisho wa kufunga mzunguko wa kwanza, wachezaji wa Yanga walipewa mapumziko ya wiki mbili, likizo ambayo itafikia kikomo Novemba 24.

Kabla ya kuondoka kurudi kwao kwa mapumziko mafupi, Brandts aliutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha Yanga inaandaliwa mechi nne za kimataifa kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga na Azam ndizo zenye jukumu la kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kwa ngazi ya klabu. Wakati Yanga ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam itakuwa na jukumu la kuahakikisha bendera ya Tanzania inapepea vema kwenye Kombe la Shrikisho Afrika.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya viwango vya ubora wa klabu barani, Simba ikiendelea kuwa juu ya klabu nyingine za Tanzania, nafasi ya tano. Orodha hiyo imetoka leo kuelekea droo ya hatua za awali za michuano ya klabu Afrika ambayo kwa mara ya kwanza kihistoria itafanyika nchini katika studio za Azam Tv, Tabata Jijini Dar es Salaam. Yanga ambayo kama Simba itashiriki Ligi ya Mabingwa — yenyewe inashika nafasi ya 12, wakati timu nyingine katika orodha hiyo ni Namungo FC wanaoshika nafasi ya mwisho, ya 75 kwa pamoja na Salitas FC ya Burkina Faso, Ahli Benghazi ya Libya na NAPSA Stars ya Zambia. Kwa msimu ujao mbali na Simba na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa, Azam FC na Singida Black Stars zitashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons

Miongoni mwa viungo wa pembeni wanaofanya vizuri ni Benodict Khalfan Ngassa ambaye amekuwa akifanya vizuri. Ngassa ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pamba Jiji na Simba SC, Khalfan Ngassa, pia ni mdogo wa kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Simba na Azam, Mrisho Ngassa anatajwa ni mmoja kati ya wachezaji wanaotazamiwa kufanya makubwa siku za usoni. Mambo Uwanjani Blog itawaletea Makala maalum ya kiungo huyo hatari ambaye ndoto zake ni kufuata nyayo za kaka yake Mrisho Ngassa. Beno Ngassa

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

Timu inaitwa Mashujaa Lake Tanganyika FC ( Mashujaa FC ) ilianza rasmi kampeni yake ya kupanda Ligi Kuu tarehe 29/9/2018 na imepanda Ligi Kuu 25/06/2023 miaka mitano ya kupambana kwenye Ligi Daraja la kwanza Championship. Timu hii inaendeshwa kwa ushirikiano wa pande mbili kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa niaba ya Wananchi wa Kigoma. Muelewe hapa maana wengi wanasema ni timu ya Jeshi asilimia 100% Nembo ya timu ni Sokwe Dume, Shujaa wa Hifadhi za Gombe na Mahale zilizopo mkoani Kigoma. Rangi ya kwanza ya jezi ya timu (first kit) ni hiyo hapo chini na kwenye nembo ya timu ni rangi za tunda la michikichi (mawese ). Hii kama njano ni mawese yaliyoganda na huo wekundu ni mawese ya moto. Ukishika tunda la Mse juu utaona wekundu na ukikata katikati utaona njano. Nyeupe ni ‘nazi’ ya Mse hizi ni alama za utajiri wa Kigoma Jezi nyingine ni blue inayowakilisha Ziwa Tanganyika na Jezi nyingine ni Nyeupe