FILAMU YA SIMBA YAZIDI KUNOGA: MZEE KINESI, HANSPOPE NAO WASIMAMISHWA.

MWENYEKITI aliyesimamishwa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage atarejea nchini Ijumaa na kulakiwa na mamia ya wanachama na ataitisha Mkutano Mkuu, ambao utafanyika Jumapili hii.

Na katika Mkutano huo, Rage amepanga kuwasimamisha Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji na baada ya hapo atasafiri kwenda nje ya nchi.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliobaki Simba SC ni Joseph Itang’are ‘Kinesi’, Said Pamba, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, Swedi Nkwabi na Zacharia Hans Poppe.

Habari za kiuchunguzi, ambazo tumezipata zimesema kwamba, Rage amekwishawasiliana na wafuasi wake wa Dar es Salaam na wameandaa mapokezi makubwa kwake atakapokuwa anawasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam Ijumaa.

Baada ya hapo, Rage ataitisha Mkutano Mkuu wa dharula Jumapili na siku hiyo atawasimamisha Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji.


“Ni kwamba tumekwishajipanga na Mwenyekiti anarudi hapa Ijumaa na Jumapili unafanyika Mkutano Mkuu, Kinesi na wenzake wote nje,”alisema mmoja wanachama wanaomuunga mkono Rage ambaye kwa sasa yuko nchini Sudan kwa shughuli zake za kisiasa.

Unaikumbuka hii? Mapema mwaka huu alisimamishwa na wanachama akiwa India na aliporejea alipokewa kifalme akaendelea kupeta.

Hatua hiyo inafuatia kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba kilichokutana juzi mjini Dar es Salaam na kufikia uamuzi wa kumsimamisha Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM, kwa kutokuwa na imani naye.

Rage anatuhumiwa kuchukua maamuzi mazito ya klabu bila kuwashirikisha wenzake na mengi yamekuwa yakiiweka klabu matatani. Pia, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za klabu na kukwamisha mambo mengi ya kimaendeleo ndani ya klabu, ikiwemo mabadiliko ya Katiba.

Baada ya kumsimamisha Rage, Kamati ya Utendaji pia ilimteua Joseph Itang’are ‘Kinesi’ kukaimu Uenyekiti wa klabu hadi hapo Mkutano Mkuu utakapofanyika.

Kinesi pia alikuwa anakaimu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa klabu, iliyoachwa wazi na Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyejiuzulu mapema mwaka huu, ambaye sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Pamoja na kumsimamisha Rage, Kamati ya Utendaji pia imewasimamisha makocha wa kikosi cha kwanza, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Msaidizi wake, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’.

Kamati imeamua kwa sasa timu itakuwa chini ya kocha wa timu ya vijana, Simba B, Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ ambaye atakuwa pia Msaidizi wa kocha Mkuu mpya wa kigeni, atakayetambulishwa Desemba 1, mwaka huu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA