AMISSI TAMBWE NAYE ATAKA KUONDOKA SIMBA
Mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Mrundi, Amissi Tambwe, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kumpa barua ya kuondoka klabuni hapo kama umemchoka na siyo kumsingizia mambo ya ajabu ambayo hajafanya na wala hatarajii kuyafanya. Tambwe ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Vital’O ya Burundi na kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao 19, hivi sasa hana amani tena katika kikosi cha timu hiyo. Hali hiyo inatokana na hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Simba kumtaja kuwa anaihujumu timu hiyo akishirikiana na baadhi ya wachezaji wenzake.