MAKALA: KINACHOTOKEA SIMBA SASA NI UHARIFU KWA WACHEZAJI, HANSPOPPE AOMBE RADHI, SPUTANZA NI WAKATI WENU SASA KUKEMEAS
AWALI wakati wa majira ya usajili nchini, timu ya kandanda
ya Simba SC iliamua kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake.
Ikiwa chini ya rais, Evance Aveva, Simba iliamua kumfuta
kazi aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mcroatia, Zdravko Logarusic na
kumuajiri, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Mabadiliko yalifanyika hasa, wachezaji wa kila aina
walisajiliwa huku wale walioshindwa kufanya vizuri msimu uliopita wakiachwa.
Lengo ya uongozi mpya ilikuwa ni kuifanya klabu ya Simba
kurudi katika hali yake ya ushindani ambayo katika kipindi cha miezi 34 sasa
imeshuka kwa kiwango kikubwa.
Sijui sana kuhusu mwanzo wa tawala nyingine katika timu hiyo
ulivyokuwa, lakini katika kipindi cha siku 14 za karibuni nadiriki kusema,
uongozi wa sasa umeanza vibaya zaidi. Sababu ni nyingi lakini kubwa zaidi ipo
katika utawala.
Simba inayumbishwa na viongozi wake wenyewe ambao wanakataa
kukubali makosa waliyofanya mara baada ya kuingia madarakani.
Kitendo cha kuwafuta uanachama baadhi ya waliokuwa wanachama
wa klabu hiyo kinawagharimu wakati huu. Ulikuwa ni uamuzi ‘ mbaya’ ambao awali
nilisema utakuwa tatizo kwa timu.
Hapa sizungumzii kuhusu sera za Aveva ambazo zilimfanya
aingie madarakani, kwani kama utazama na kugusa huko vile ilivyo sasa ‘
ameshindwa vibaya’, alikuwa na sera mbovu, lakini si hivyo ‘ sera ya pointi 3’
imekufa, hivyo ni lazima zitazamwe sababu zilizofanya sera hiyo kutokuwa na mafanikio.
Katika mchezo wa kwanza wa msimu huu, Simba ilicheza na
Coastal Union ya Tanga katika uwanja wa Taifa, ilionekana kama vile mambo
yatakwenda sawa msimu huu baada ya Shaaban Kisiga kufunga bao la ‘ mkwaju wa
penalti’.
Lilikuwa bao la kwanza la msimu kwa Simba, na lilifungwa na
mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kikosini tena ‘ kwa kutumia maarifa binafsi’.
Amis Tambwe akafunga bao la pili, lakini mambo yalikuwa
magumu dakika 25 za mwisho. Coastal walichomoa mabao yote na kutengeneza sare
ya kufungana mabao 2-2. Halikuwa tatizo, hakukuwa na hujuma.
Hanspoppe: Mzee mzima umechemsha kabisa kutokana na kauli zako zisizo za kitaalamu kuhusu Kiemba, Chanongo na Kisiga wakati jamaa wanajituma sana
Mchezo wa pili ulikuwa ni dhidi ya Polisi Morogoro, pia
ulipigwa katika uwanja wa Taifa. Simba iliongoza kwa bao la mshambulizi,
Emmanuel Okwi.
Ndani ya nusu saa ya mchezo. Mshambulizi wa zamani wa Simba
Danny Mrwanda akiitumia vizuri ‘ pasi ya kupenya’ iliyopigwa na kiungo Salum
Machaku na kuisawzishia timu yake dakika tano tu mara baada ya kuanza kwa
kipindi cha pili.
Mechi ikamalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1. Hapa kidogo
maswali yakaanza kujitokeza, kiwango kibovu kutoka kwa baadhi ya wachezaji
kilifanya wengi kuanza kujiuliza kulikoni.
Katika hali ya kutojiamini, ama kutoheshimu timu pinzani.
Uongozi wa Simba ulikaa chini na kufikia mwafaka wa kuhitisha kikao cha siri
kati ya utawala, benchi la ufundi na wachezaji.
Bila uoga baadhi ya wachezaji walisema kuwa matokeo ya sare
mbili mfululizo yaliletwa na ushirikiano mdogo uliopo katika timu.
Hawakugusia mambo yaliyopo katika uongozi bali walisema ‘
wachezaji kwa wachezaji’ hawapeani ushirikiano ule wa kimpira wakiwa uwanjani.
Ilikuwa ni hoja ambayo ndani yake ina mantiki kwa sababu
kuna baadhi ya viongozi wameonekana kuwagawa baadhi ya wachezaji na kuwapendelea
wengine kwa sababu tu mchezaji Fulani hajasajiliwa na ‘mtu/watu fulani’.
Baada ya kikao hicho mambo yalikwenda vilevile. Mchezo wa
tatu ulikuwa ni dhidi ya Stand United ya Shinyanga ambao nao ulifanyika katika
uwanja wa Taifa.
Kisiga akitokea benchi kuchukua nafasi ya Said Ndemla
aliyeumia alifunga bao lake la pili msimu huu, pia lilikuwa bao la mkwaju ‘
uliokufa’.
Katika ligi ambayo mabao kadhaa yamefungwa kwa mipira ya
adhabu ndogo, Kisiga anaweza kuipa Simba pointi ‘ tatu za kwanza’ msimu huu kama
tu safu ya ulinzi isingeendeleza ‘ tabia yao ya kukubali kuruhusu bao la
kuswazishwa’.
Mwishoni mwa mchezo Stand walichomoa na kutengeneza sare ya
Tatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani’.
Katika mchezo wowote huwa tunasema; ‘ asiyekubali kushindwa,
si mshindani’, lakini katika fikra za kishabiki, matokeo ya Simba yalipangwa.
Hivyo ndivyo wanavyoamini baadhi ya viongozi. Nahodha,
Joseph Owino aliwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Stand na nafasi yake
kuchezwa na chipukizi, Joram Mvegeke.
Sijui kama yalikuwa ni mapendekezo ya Phiri mwenyewe kama
mkuu wa benchi la ufundi, au ni muendelezo wa makocha ‘ dhaifu wa kigeni’ ambao
wanaendeshwa ‘ kwa rimoti’ na baadhi ya watu wenye kuwashikilia?.
Kama tatizo la kwanza ilionekana ni Owino, Simba hawakung’amua
chanzo cha tatizo lenyewe.
Je, baada ya Owino kuwekwa benchi, safu ya ulinzi ilifanya
kazi nzuri zaidi?. Matokeo yalikuwa ni ‘ yale yale tu’. Mchezaji pekee ambaye
hajakosekana katika safu ya ulinzi ya Simba msimu huu ni Hassan Isihaka.
Kiwango chake ni kizuri lakini kama sababu ni hujuma,
wengine wote waliofanyiwa mabadiliko hawakuleta afadhali yoyote hadi pale Owino
alirudishwa katika mchezo dhidi ya Yanga ambao ni pekee Simba hawakufunga bao
wala kuruhusu goli msimu huu.
Kihistoria, Simba ilipaswa kuchukua pointi tatu dhidi ya
Polisi Moro kwa sababu huwa hawana uwezo wa kuifunga timu hiyo ya Morogoro
ikiwa nyumbani katika miaka ya karibuni.
Sare dhidi ya Coastal ni kielelezo cha ugumu wa ligi ya
msimu huu, sare ya Stand ni matokeo ya soka tu. Huku suluhu dhidi ya Yanga
ilichukuliwa kama ‘ mwisho wa matatizo’. Hawakujua, kumbe ni mwanzo wa kuelekea
kipigo cha kwanza msimu huu.
Wakati Fulani msimu uliopita ulipokuwa ukielekea mwishoni,
niliwahi kuhoji kiwango cha kiungo Haroun Chanongo. Ukweli wakati ule wa mchezo
dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1 niliamini kuwa,
Chanongo ni mchezaji mwenye ‘ tabia ya kupanda na kushuka kwa kiwango chake’.
Lakini kuanzia msimu huu, mchezaji huyo amekuwa juu, lakini
ametimuliwa kambini kwa sababu za kudaiwa kuchangia matokeo mabaya ya timu.
Kivipi?
Okwi alifunga bao la kuongoza kwa timu yake na kuifanya iwe
mbele kwa bao 1-0 katika uwanja ambao wameishinda, Tanzania Prisons mara mbili
tu katika kipindi cha miaka 14 sasa.
Zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika Prisons
waliswazisha. Simba imepata pointi ya kwanza katika uwanja wa ugenini msimu huu
baada ya kufungana bao 1-1 na Prisons lakini hilo limeambatana na kusimamishwa
kwa baadhi ya wachezaji.
Chanongo, Kiemba na Kisiga. Lakini katika hali ya kimpira
tuhuma hizo si za kweli zaidi ya ‘ chuki binafsi alizonazo’ mwenyekiti wa
kamati ya usajili kwa wachezaji hao ambao hakuwasajili yeye.
Haruna Chanongo msimu huu amerejea katika kiwango chake tofauti na viongozi wanavyodai hadi kumsimamisha
Majuzi alisikia mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili akisema
kuwa kila anapopangwa Kiemba timu yao haishindi. Je, huu ndiyo weledi wa
kiuongozi. Ule mgawanyiko ambao wachezaji waliusema katika kikao unaletwa na
viongozi kama hawa ambao wanasema tu wachojisikia.
Nathubutu kusema kuwa baada ya sare tano mfululizo, Simba itapigwa
na Mtibwa Sugar wikiendi ijayo na baada ya hapo atakayefuata ni kocha Patrick
Phiri.
Lakini Simba SC inaharibiwa na hao jamaa zao wenyewe, ‘ Watu
wakubwa’. Wakati wa uongozi wa Mh. Aden Rage nilikuwa nikipenda kutumia sentesi
ya ‘ Mtu mkubwa ni Mwanafunzi’, hutamani vitu vingi zaidi.
Labda Phiri apange wachezaji wote waliosajiliwa na ‘ Mbwana
Mkubwa’ ndipo Simba itashinda!!. Nyakati za furaha zimepotea klabuni huku ndani
ya uwanja matokeo yakiwa ‘ hovyo’.
Msiwape lawama ‘ wale-Simba Ukawa’ ambao hawajulikani
wanaishi wapi, ‘ adui wa kwanza wa Simba ni Pesa’, Si Kiemba, Kisiga wala
Chanongo. Niliwahi kuandika ‘ Phiri atafukuzwa kazi Simba SC….
Phiri yupo katika ‘ shinikizo la
chinichini’ hivi sasa. Hakuna, Simba ukawa ila kuna watu ndani ya Simba yenyewe
wanataka Simba ifungwe sasa na si kutoa sare, unajua ni kwa nini? Mtu mkubwa ni
Mwanafunzi tu.