KIONGERA, IVO WATOSWA SIMBA.

Kiungo mshambuliaji Raphael Kiongera na kipa Ivo Mapunda wameachwa kwenye kikosi cha Simba kinachoondoka leo kwenda Afrika Kusini kuweka kambi ya muda kujiandaa na mechi yao dhidi ya watani, Yanga, Oktoba 18.

Kiongera na Ivo watakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu na Mkenya huyo aliyeumia goti ataruhusiwa kurudi uwanjani Desemba wakati Ivo aliumia kidole kidogo cha mkono.

Beki na nahodha wa kipindi kilichopita, Nasoro Masoud ‘Chollo’ ambaye ameanza mazoezi ya gym jana huenda akawamo kwenye msafara huo, ingawa uwezekano wa kucheza mechi hiyo ni mdogo.


Mbali na wachezaji hao, wengine ambao hawataungana na kikosi cha kocha Patrick Phiri ni wale walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ambao ni Said Ndemla, Haruni Chanongo, Amri Kiemba, Jonas Mkude na kinda Joram Mgeveke.

Hata hivyo, wachezaji hao wataungana na wenzao baada ya mechi yao dhidi ya Benin itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha Phiri aliliambia gazeti hili kuwa kambi hiyo itakuwa na faida kupanga mipango na mikakati ya ushindi katika mechi hiyo baada ya kutoka sare katika mechi zao tatu ambazo wameambulia pointi tatu.

“Tunaenda kuweka kambi ya ushindi, naamini wachezaji wangu watakuwa katika wakati mzuri wa kujiandaa na kujijengea uwezo mkubwa ili kuhakikisha tunaifunga Yanga, huu ni mchezo mgumu na unahitaji maandalizi makubwa na yenye utulivu.

“Nimekubaliana na uongozi katika kikao cha pamoja na tumeridhia kwa pamoja kuwa tukaweke kambi Afrika Kusini. Nitaondoka na wachezaji wote kasoro wale tu ambao wapo Stars na wale ambao ni majeruhi,” alisema.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA