AMISSI TAMBWE NAYE ATAKA KUONDOKA SIMBA

Mfungaji bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara,  Mrundi, Amissi Tambwe, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kumpa barua ya kuondoka klabuni hapo kama umemchoka na siyo kumsingizia mambo ya ajabu ambayo hajafanya na wala hatarajii kuyafanya.

Tambwe ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Vital’O ya Burundi na kufanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao 19, hivi sasa hana amani tena katika kikosi cha timu hiyo.

Hali hiyo inatokana na hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Simba kumtaja kuwa anaihujumu timu hiyo akishirikiana na baadhi ya wachezaji wenzake.


Tambwe amesema kuwa kama wamemchoka ni bora wakampatia barua ya kuachana na klabu hiyo na siyo kumchafulia jina.
Alisema amechoshwa na tuhuma hizo ambazo zinamfanya atumie muda mwingi kuzitafakari japokuwa hazina ukweli wowote na kushindwa kufikiria mambo ya msingi yatakayomwezesha kufanya vizuri katika mechi zijazo za timu hiyo.

“Sasa ndiyo naamini yale niliyokuwa naambiwa na wachezaji wenzangu wa Burundi waliowahi kuzitumikia timu za Tanzania kuwa hata ufanye mema mangapi ipo siku utadharaulika na utaonekana mtu usiyefaa kabisa.

“Mema yote na kujitolea kwangu uwanjani nilikofanya msimu uliopita ili kuhakikisha tunafanya vizuri leo hii naonekana sifai, eti naihujumu Simba kwa sababu tu sifungi, hakika naumia sana.

“Katika soka kuna mambo mengi ambayo yanaweza kumkuta mchezaji, kutofunga kwangu siyo kwamba nafanya makusudi nimekuwa nikijitahidi sana kutafuta nafasi lakini mambo yanakuwa magumu kwa sababu timu nyingi zimejiandaa vizuri na wachezaji wengi msimu huu wapo makini sana na mimi ndiyo maana hali hiyo imetokea hivyo sipaswi kulaumiwa.

“Kama wanaona nafanya makusudi basi wanipe barua ya kuachana na mimi na siyo wasinichafulie jina langu kwa kunisingizia mambo ambayo sijafanya,” alisema Tambwe ambaye msimu huu amefunga bao moja katika mechi nne alizocheza.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA