YANGA YAIFUATA SIMBA ZENJI
Wakati Simba imechagua Zanzibar kuwa kambi yake, kikosi cha cha mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga, nacho kinatarajiwa kwenda kujichimbia mjini humo kwa ajili ya kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa ligi hiyo itakayoanzia Septemba 12, mwaka huu. Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, alisema jana kuwa wameamua kwenda visiwani humo ili kujiimarisha kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi. Tiboroha alisema kwamba kambi hiyo itakuwa ya siku saba na lengo ni kuwafanya wachezaji waliobakia nchini kujijenga na kuwa imara tayari kukabiliana na ushindani wa mechi za ligi hiyo. "Tunataka wachezaji wenzao ambao wako na timu za taifa wakirudi wote wawe fiti kwa ajili ya kushindana ligi itakapoanza," alisema Tiboroha.