CHAMBERLAIN AIWEZESHA ARSENAL KUICHAPA CHELSEA 1-0



Mabingwa Kombe la FA Arsenal waliwalaza mabingwa wa ligi Chelsea 1-0 katika mechi ya Community Shield, ambayo hutumiwa kufungua msimu mpya wa ligi Uingereza, iliyochezewa Wembley Jumapili.

Bao safi la Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya 24 lilitosha kuamua mshindi wa mechi hiyo iliyochezewa katika anga yenye jua kiasi.

Mchezaji huyo wa miaka 21 alipokea pasi kutoka kwa Theo Walcott, akambwaga difenda wa Chelsea Cesar Azpilicueta before na kisha kutuma kombora kona ya juu ya goli, kombora ambalo Thibaut Courtois hakuweza kulizuia.

Ilikuwa mara ya kwanza katika majaribio 14 kwa meneja wa Arsenal Arsene Wenger kumpiku mkufunzi wa Chelsea Jose Mourinho na matokeo hayo yaliwapa matumaini kwa wapinzani wa Chelsea kwamba huenda wasiwe na mteremko kama waliokuwa nao msimu uliopita.


Chelsea walishinda taji Mei wakiwa alama nane mbele ya Manchester City waliomaliza wa pili na wanapigiwa upatu sana na wengi kuhifadhi taji hilo, kwenye msimu mpya utakaoanza Jumamosi.
Arsenal walitawala kipindi cha kwanza na walizawadiwa na bao la Oxlade-Chamberlain.

Chelsea walijaribu kujiimarisha kipindi cha pili, wakimwingiza Radamael Falcao, waliyemchukua majuzi kwa mkopo, kujaza nafasi ya mshambuliaji wao Loic Remy na wakamtoa Ramires na kumuingiza Mbrazil mwenzake Oscar.

Golikipa Petr Cech, aliyechezea Chelsea karibu mechi 500 kabla ya kujiunga na Arsenal na alikaribishwa kwa shangwe na mashabiki wa pande zote kabla ya mechi kuanza, alitumia haiba ya hali ya juu kuzima frikiki ya Oscar dakika ya 69.

Chelsea walisaka bao la kusawazisha kwa udi na uvumba lakini hawakuweza kutishia wapinzani wao, huku wakionekana kumkosa mshambuliaji Mhispania Diego Costa ambaye hakuweza kucheza baada ya kuumia.
Winga Mbelgiji Eden Hazard alituma mpira juu ya wavu katikati ya kipindi cha kwanza, jambo la kushangaza kwa mchezaji huyo aliyetawazwa mchezaji bora wa mwaka Uingereza msimu uliopita.

Arsenal walipumzisha wachezaji wengi nyota akiwemo mshambuliaji wao Alexis Sanchez aliyerejea mazoezini akiwa amechelewa baada ya kusaidia Chile kushinda Copa America.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI