MAKALA: YANGA SC NDIYO MABINGWA WA KIHISTORIA WA NGAO YA HISANI
Barthez alipangua penalti za beki raia wa Ivory Coast Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Ame Ali 'Zungu', wakati kipa wa Azam FC Aishi Manula naye alicheza penalti ya nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Penalti za Yanga SC zilifungwa na Haruna Niyonzima 'Fabregas', Deus Kaseke, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na Kelvin Yondani aliyefunga ya mwisho.
Penalti za Azam FC zilikwamishwa wavuni na Kipre Thetche, nahodha John Raphael Bocco, Himid Mao, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Jean Bapstita Mugiraneza 'Migi', ushindi huo wa Yanga SC ni sawa na kulipiza kisasi baada ya kufungwa kwa penalti 5-4 katika robo fainali ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati (kombe la Kagame) Julai 29 mwaka huu uwanja huo huo wa Taifa baada ya sare ya 0-0.
Katika dakika 90 za mchezo huo wa jumamosi iliyopita timu zote zilishambuliana kwa zamu na kosakosa zilikuwa kila upande lakini dakika za mwishoni, Yanga SC walikuwa wakali zaidi.
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alionekana kabisa akijiangusha kupoteza muda ili kupunguza kasi ya Yanga SC, dakika za mwishoni beki Kelvin Yondani alicheza kwa kiwango kikubwa na dakika ya 37 aliitokea pasi ya Mzimbabwe Thabani Kamusoko na kumchambua vizuri kipa Aishi Manula lakini beki Shomari Kapombe akabinuka tik tak kuuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
Wachezaji wote wa Yanga wakiwa na kocha wao Mbrazil Marcio Maximo mwaka jana 2014 wakifuarhia Ngao ya Hisani waliyoichukua baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-0
Hii inakuwa mara ya tano Yanga SC kutwaa Ngao ya Hisani ikiwa ni rekodi, baada ya kuifunga Simba SC mara mbili mwaka 2001 mabao 2-1 na 2010 penalti 3-1 baada ya sare 0-0 ndani ya dakika 90, miaka mitatu mfululizo 2013, 2014 na 2015 mara zote ikiifunga Azam FC.
Yanga SC iliifunga Azam FC bao 1-0 na kutwaa Ngao ya Hisani mwaka 2013 na kuendeleza ubabe huo 2014 ilipoifunga tena Azam FC mabao 3-0 na kushuhudia tena jumamosi iliyopita ikiifunga kwa penalti 8-7.
Simba SC inafuatia ikiwa imetwaa mara mbili mwaka 2011 wakiifunga Yanga SC 2-0 na mwaka 2012 wakiifunga Azam FC 3-2, wakati Mtibwa Sugar ni timu nyingine iliyowahi kutwaa Ngao ya Hisani mwaka 2009 ikiifunga Yanga SC 1-0.
Yanga wanakuwa mabingwa wa kihistoria wa Ngao ya Hisani sawa na ubingwa wa ligi kuu bara ambao wao wanaongoza wakichukua mara 25, mwaka 2013 Yanga ilidhihirisha kwamba wao ni wababe baada ya kuilaza Azam FC 1-0 , goli likifungwa na kiungo Salum Telela.
Na mwaka 20154 iliendeleza tena ubabe kwa kuichapa Azam FC mabao 3-0, magoli mawili yaliwekwa kimiani na Mbrazil Geilson Santana Santos 'Jaja' na lingine likifungwa na winga Simon Msuva.
Kumalizika kwa mchezo huo wa Ngao ya Hisani kunadhihirisha kuanza kwa ligi kuu bara na takwimu zinaonekana kwa timu mbili zilizocheza mechi hiyo.
Licha kwamba wachezaji wake waliocheza mechi hiyo kuzidi kupata uzoefu, lakini kila timu imenufaika na kikosi chake kwakuwa makocha wa timu zote wamepata muda wa kujua mapungufu ya timu zao.
Yanga SC imeonekana kuimarika mno kutokana na wachezaji wake kucheza kwa kujiamini na kutafuta nafasi za kufunga, kikosi cha Yanga kilichoanza katika mchezo huo kimeonyesha kinaweza kupambana.
Azam FC ambao ni mabingwa wa Afrika mashariki na kati (kombe la Kagame) bado wameshikilia rekodi yao ya kucheza mechi 13 bila kuruhusu hata bao moja, Azam FC ni timu inayoonekana kutoa ushindani mkubwa na kwa vyovyote ligi inayotarajia kuanza juma lijalo itakuwa na ushindani mkubwa.
Kikosi cha Yanga SC ambacho kimeweka rekodi ya kunyakua mara tano kombe la Ngao ya Hisani
Yanga SC iliyotwaa Ngao ya Hisani ni timu ngumu ambayo sidhani kama itashindwa kutetea ubingwa wake wa bara, wachambuzi wa soka Afrika mashariki wamekiri Yanga SC ni timu bora kwani ilipokutana na Azam FC katika mchezo wa robo fainali kombe la Kagame ilionyesha kiwango kikubwa.
Hata mchezo wake wa jumamosi iliyopita Yanga ilionekana kuizidi Azam FC kila idara na kama si juhudi za mabeki wake basi mchezo huo ungemalizika mapema bila hata ya kupigiana penalti, shukrani nyingi zimwendee kocha mkuu wa timu hiyo Mholanzi Hans VAN der Pluijm.
ORODHA WA MABINGWA WA NGAO YA HISANI TANGIA MWAKA 2001
2001. Yanga SC 2-1 Simba SC
2009. Mtibwa Sugar 1-0 Yanga SC
2010. Yanga SC 0-0 Simba SC
(Yanga ilishinda kwa penalti 3-1).
2011. Simba SC 2-0 Yanga SC
2012. Simba SC 3-2 Azam FC
2013. Yanga SC 1-0 Azam FC
2014. Yanga SC 3-0 Azam FC
2015. Yanga SC 0-0 Azam FC
(Yanga ilishinda kwa penalti 8-7.
Mbali na Pluijm, kamati ya usajili nayo ilipaswa kupongezwa hasa baada kukamilisha vema ujio wa wachezaji wake wapya ambao wameonekana kuwa na viwango bora, Yanga SC haikubahatisha kwani ilistahili matokeo mazuri tangia mwanzo.