MAKALA: WAKUBWA WANAPOAMUA KWA MECHI MOJA, WAKUSAJILI AMA WAKUTIMUE

Na Prince Hoza



SOKA ni mchezo wa bahati, unaweza kumuona mchezaji fulani aa kiwango kizuri kwa kucheza vizuri kwenye mechi moja na ukamuamini mpaka kufikia hatua ya kumpa mkataba, lakini anapocheza mechi nyingine ya pili anachemsha na baadaye mnaanza kulaumiana wenyewe kwa wenyewe kwanini mmepitisha usajili wake.

Ndivyo ulivyo mchezo wa soka, bahati huchukua nafasi yake, lakini pia kuna bahati nzuri na bahati mbaya, katika mcheZo wa soka mchezaji anaweza akawa na sifa nyingi huko alikotoka na akasajiliwa timu nyingine ili aonyeshe makali yake ila kwa bahati mbaya akashindwa kuonesha kile alichokuwa akikionyesha mwanzo.

Mchezaji huyo yapaswa umpe muda mwingine ili ujiridhishe naye, lakini ukimkatia tamaa kwa mechi moja tu, unaweza kuchuma dhambi za bure na kumrudisha kwao.

Simba SC imeshawarudisha makwao wachezaji zaidi ya wawili, ilianza na Daniel Akufor baadaye Gervais Kago na sasa Papa Niang, na tayari imewaleta nchini washambuliaji wengine wawili ambao ni Pape Abdoulaye N'Daw raia wa Senegar na straika raia wa Mali Makan Dembele.


Ngojeni niwape mkasa kidogo kabla sijaingia kwenye mada halisi, Wakati mimi nikicheza soka nikiwa bado sijamaliza masomo ya shule ya msingi, niliwahi kwenda likizo kijijini kwetu ambako ilinilazimu kuungana na vijana wadogo wenzangu na kujumuika nao kwenye michezo hasa soka.

Nikiwa mazoezini kila siku niliwaonyesha vitu vyangu, siyo siri mpira niliujua sana isipokuwa sikucheza ligi kuu, nilikuwa nacheza nafasi ya ushambuliaji, na nilitisha kwa kutupia magoli, mabeki walishindwa kunidhibiti kutokana na umahiri wangu wa kuchomoka na mpira.

Nilikuwa na kasi ya aina yake, lakini ilikuwa mazoezini tu, mashabiki wa timu yetu walinipenda sana, kuna siku moja tulicheza mechi ya kirafiki na timu ya kijiji kingine cha jirani, mimi nilipangwa kuanza katika kikosi cha kwanza.

Basi tumaini la timu yetu nilikuwa mimi, lakini cha kushangaza mashabiki wa timu yetu walikuwa wakinizomea kwa kuwa nilicheza chini ya kiwango, kelele nilianza kuzisikia wakitaka nitolewe aingie mchezaji mwingine ambaye hakuwa tegemeo kama nilivyokuwa mimi, walidhania bahati inacheza.

Kwakweli siku hiyo nilionekana sifai, lakini mpira ulikuwa mapumziko tulielekea walipokaa mashabiki wetu na kusikiliza mawaidha, kuna shabiki mmoja alishauri nitolewe, lakini kuna mwingine ambaye huwa anajitoleaga kununua vifaa vya timu alishauri niendelee kipindi cha pili huenda nitabadilika.

Mungu mkubwa, kipindi cha pili nilifanikiwa kufunga magoli mawili na kusaidia kutengeneza lingine moja, nilishangiliwa na mashabiki wetu akiwemo yule aliyetaka nitolewe, mpira ulimalizika timu yangu ikiwa mbele kwa mabao 4-1, siku hiyo hiyo mashabiki walinichangia nauli ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na shule.

Straika huyu ametua Simba SC baada ya kutemwa Papa Niang, naye anaweza kutimuliwa baada ya mechi moja

Simba SC nayo ilimleta nchini mdogo wake mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Senegar Mamadou Niang, Mamadou anakumbukwa vema na Watanzania hasa baada ya kututungua mara mbili wakati Senegar ikiilaza Tanzania mabao 4-0, mchezo wa makundi mataifa Afrika mwaka 2006.

Papa Niang haikuwa ngumu kueleweka kwa vile ni ndugu wa mchezaji maarufu, alitua Simba SC kwa sifa lukuki tulizoaminishwa, tuliambiwa anajua kufunga, yeye akili zake na goli tu, moja kwa moja alipangwa kwenye mchezo wa kirafiki Jumatatu iliyopita dhidi ya Mwadui FC uliofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mwadui FC timu iliyopanda daraja msimu uliopita hivyo msimu ujao itashiriki ligi kuu bara ilitumia mechi hiyo kama sehemu ya kukijaribu kikosi chake chenye wachezaji wapya iliowasajili, Mwadui inanolewa na mchezaji wa zamani na kocha wa Simba Jamhuri Kihwelu 'Julio'.

Hivyo alihakikisha timu yake ya sasa Mwadui inaizuia timu yake ya zamani Simba, kwahiyo mpira ulikuwa wa kukamiana.

Simba iliingia uwanjani kwa lengo la kumjaribu mshambuliaji mpya Papa Niang, huenda kelele za mashabiki wa Yanga zilimtisha, Niang kwa bahati mbaya mpira ulimkataa, alishindwa kufunga goli hata moja, kocha Dylan Kerr aliamua kumtoa baada ya kucheza dakika 45 za kwanza, hakumvumilia.

Nilidhani mchezaji huyo atapewa muda ili aweze kubadilika kama mimi, lakini hii ndiyo kawaida yetu Watanzania hatuna subira, Niang kachinjiwa baharini, ni ustaarabu wetu wa kujiamulia, hata huko mtaani mtu anaweza kuuawa hivi hivi kwa kupigiwa kelele za wizi basi wananchi hawataki kuchunguza kwanza wanaanza kumshambulia na kumchoma moto hadi kufa.

Baadaye unaambiwa huyo aliyeuawa kumbe ni msoma mita wa Tanesco kila mtu anashangaa, Watanzania tunajiamulia bila kuchunguza kwanza, tunajiamulia bila kumpa muda muafaka.

Papa Niang hakustahili kurejeshwa haraka kwao kwa kukosea mechi moja tu, hata Azam FC walimvumilia beki wao Serge Wawa Pascal ambaye kwa sasa ndiye mhimili mkuu wa timu hiyo, mechi moja imeamua kumwondoa Niang, lakini mechi moja hiyo hiyo ndiyo iliyompa mkataba wa miaka miwili kipa raia wa Ivory Coast Vincent Angban.

Kipa huyo alidaka vizuri kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya SC Villa ya Uganda uliofanyika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Yanga SC walimsajili beki huyu raia wa Ghana, Joseph Zuttah lakini baada ya kuonekana kwenye mechi moja tu, waliamua kumkata

Simba ilishinda 1-0 goli lililofungwa na Awadh Juma katika dakika za lala salama, mchezo huo wa kuhitimisha tamasha la Simba Day linalotekelezwa kila ifikapo Agosti 8.

Mchezo huo pia ndio ulioamua hatma ya mlinda mlango Ivo Mapunda ambaye alitupiwa virago, usajiliwa Angban haukuwa na shaka hata kidogo lakini ifahamike kuwa soka ni mchezo unaotegemea bahati.

Lakini mechi nyingine moja ya kirafiki ya kimataifa kati ya Simba na URA ya Uganda nayo ilimuongezea umaarufu mshambuliaji raia wa Burundi Kevin Ndeyisenga mpaka kupelekea kupondishwa kwa dau lake la usajili tofauti na makubaliano ya awali, Ndeyisenga alifunga goli, lakini mechi zuri sana, ila ni mechi moja tu ndiyo iliyojaji uwezo wake na wengi kumkubali.

Na siku zote bahati zipo mbili tu hapa duniani, yaani kuna bahati nzuri na bahati mbaya, na mwanaadamu yeyote yule anaweza kuzipia bahati zote hizo lakini kikubwa ni uvumilivu.

Viongozi na wapenzi wa Simba SC mnapaswa kuwa wavumilivu katika kipindi kama hiki ili kunusuru mamilioni ya fedha yanayotumika kuwaleta na kuwarudisha wachezaji wapya wa kigeni wanaokuja kufanyiwa majaribio.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA