Mike Tyson apata shavu kwa Rais Trump
Bondia maarufu wa zamani, Mike Tyson, amezua gumzo baada ya kuonekana akiandamana na Rais wa Marekani, Donald Trump, katika safari iliyohusisha helikopta ya urais, Marine One, na ndege ya Air Force One. Tyson alionekana akitembea na Trump katika bustani ya Ikulu ya Marekani kabla ya kupanda Marine One kuelekea kituo cha kijeshi cha Joint Base Andrews. Baadaye, walipanda Air Force One kuelekea Syracuse, New York, kwa mkutano wa kisiasa. Kabla ya safari hiyo, Trump alimtambulisha Tyson kwa waandishi wa habari huku akitania kwamba hatapigana naye siku hiyo, akieleza kuwa wamekuwa marafiki kwa muda mrefu. Urafiki wao ulianza miaka ya 1980, wakati Trump alipohusika katika kuandaa mapambano ya ndondi ya Tyson huko Atlantic City.