Kocha Yanga ajitetea, kipigo cha Simba, amtaja huyu!
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, ameweka wazi kuwa majeraha aliyoyapata kiungo wa kimataifa wa Kenya, Duke Abuya, katika kipindi cha kwanza ndiyo yaliyokuwa nukta ya mabadiliko (turning point) iliyopelekea kupoteza mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba SC.
Abuya alilazimika kutolewa uwanjani mapema katika dakika ya 25 kufuatia kupata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto wakati Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0, kabla ya Simba SC kupambana na kupindua meza na kuibuka na ushindi wao wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya watani zao tangu mwaka 2023.
"Kwa bahati mbaya tulimkosa Duke na nafikiri hapo ndipo mchezo ulipobadilika. Yeye ni mchezaji muhimu sana katika timu yetu," alisema Mngqithi kupitia Eleven Eleven TV.
"Kwa maoni yangu, mchezo ulipotelea kwenye ule mabadiliko ya Duke kwa sababu safu yetu ya kiungo ilikuwa imara sana. Timu ilikuwa ikicheza vizuri mno, lakini kwa bahati mbaya unapomkosa mchezaji nguzo mapema hivi kwenye mchezo, inabidi ujitoe kwa kiwango kikubwa sana kusawazisha pigo hilo."
