WAKATI Yanga ikiwa katika maandalizi ya mwisho kuwavaa Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, jambo jipya limeibuka kuwa yule mshambuliaji wake hatari, Kpah Sherman raia wa Liberia, anatuhumiwa kutoroka kazini nchini Cyprus Kaskazini. Taarifa kutoka Cyprus Kaskazini barani Ulaya kwa mmoja wa Watanzania wanaoishi nchini humo zimeeleza vyombo vya habari nchini humo, vimeripoti kuwa Mliberia huyo atafunguliwa mashitaka baada ya kutorokea Tanzania. “Nimesikia huyo mchezaji yuko huko nyumbani, ila huku vyombo vya habari vya hapa vimeripoti timu yake ina mpango wa kufungua kesi Fifa kuelezea kuhusiana na kutoroka kwake,” alisema Mtanzania huyo anayeishi nchini humo. Juhudi za kuwapata viongozi wa Yanga ilikuwa ni ‘sheedaa’, imeelezwa Mwenyekiti Yusuf Manji yuko nje ya nchi na katibu mkuu mpya, hajaingia ofisini rasmi. Uongozi wa Klabu ya Centikaya TSK ya Cyprus, umethibitisha kushitushwa na taarifa za Sherman kuondoka nchini humo akidai ana matatizo ya kifamilia.