MAKALA: NI SIMBA AU YANGA ATAKAYECHEKA TAIFA LEO?

Amisi Tambwe alifunga mara mbili katika muda wa dakika 45 za kipindi cha kwanza katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, mwishoni mwa Disemba ,2013 kisha kiungo, Awadh Juma akafunga bao lingine na kutengeneza ushindi wa aina yake kwa timu yao ya Simba SC dhidi ya mahasimu wao wa soka nchini Yanga SC.


Emmanuel Okwi alifunga ‘ bao kali’ katika mchezo huo dakika za mwishoni mwa mchezo ambao ulikuwa ni wa kwanza kwake katika timu ya Yanga ambao walimsaini kwa usajili uliozua utata mkubwa kutoka SC Villa ya Uganda.



Yanga walipoteza mchezo huo kwa kulazwa mabao 3-1, na siku chache baadaye aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Ernie Brandts alifutwa kazi licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili siku kadhaa kabla ya mchezo huo.

Katika michezo mitatu ya mwisho ya ligi kuu, timu hizo hazijafungana. Zilitoka sare ya kufungana mabao 3-3, Oktoba, 2013, Simba walikuwa nyuma kwa mabao 3-0 hadi nusu ya kwanza ya mchezo ilipomalizika, lakini wakakomboa mabao yote hayo katika dakika 45 za kipindi cha pili, zikatoka sare ya kufunga bao 1-1, Mei, mwaka huu safari hii Yanga wakichomoa dakika za mwisho, na katika mchezo wa mwisho walipokutana mwezi Oktoba mwaka huu timu hizo hazikufungana.

SSERUNKUMA, OKWI, TAMBWE…

Hakuna anayejua ni wachezaji gani kocha Patrick Phiri wa Simba ambao atawaanzisha katika safu ya mashambulizi, lakini wengi upande wa Simba watapenda kuona washambuliaji watatu wa kimataifa wakianza katika safu yao ya mashambulizi.

Tambwe kama mshambulizi wa kwanza, Okwi akishambulia kutokea upande wa kushoto na nyota mpya, Danny Sserunkuma akishambulia kutokea upande wa kulia katika mfumo wa 4-3-3.

MRWANDA, NGASSA & MSUVA…

Wakati mashabiki wa Simba wakitamba na safu yao ya mashambulizi, Marcio Maximo kocha wa Yanga anaweza kufanya uamuzi mpya katika safu ya mashambulizi ya timu hiyo kwa kuwaanzisha washambuliaji watatu wa Kitanzania. Danny amesajiliwa kutoka Polisi Morogoro na atakuwa akicheza mchezo wake wa kwanza akiwa mchezaji wa Yanga, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva wanaweza kutengeneza safu mpya ya mashambulizi isiyo na mchezaji wa kigeni katika kikosi cha kwanza.

JONAS MKUDE, EMERSON, TIMU ITAKAYOTAWALA KIUNGO INAWEZA KUSHINDA?.

Bado haitatosha kwa wachezaji wa nafasi ya kiungo wa kila timu kutawala tu eneo hilo muhimu katikati ya uwanja na kuchukulia kama sababu ya kupata matokeo bora.

Katika mchezo wa mwisho baina ya timu hizo, Jonas Mkude, Amri Kiemba na Said Ndemla walianza katika safu ya kiungo ya Simba, wakati Mbuyu Twite, Hassan Dilunga na Haruna Niyonzima walianza upande wa Yanga. Simba walitawala robo saa ya kwanza lakini alipokuja kuumia Ndemla katika robo ya mwisho ya mchezo na kuingia Shaaban Kisiga,

Yanga walionekana ‘ kuuchukua mchezo’. Lakini hakuna nafasi muhimu iliyotengenezwa na wachezaji wa nafasi ya kiungo kwa kila upande. Mkude alikuwa imara na alijaribu kupita katika kila njia ya Niyonzima, Mbuyu alifanya hivyo mara mbili zaidi kwa kuwa ilibidi awatazame, Kiemba na Okwi.

Yanga watakuwa wakimkaribisha kikosini mwao kwa mara ya kwanza kiungo, Mbrazil, Emerson de Oliveira, kwa maana hiyo kuna uwezekano mkubwa wa Mbuyu kurudishwa kucheza nafasi ya ulinzi wa pembeni-kulia ili kumpisha mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo-mlinzi kucheza sambamba na Niyonzima pamoja na Dilunga katika mfumo wa 4-3-3.

Itakuwa mechi ngumu kwa Emerson na atakuwa mchezaji anayefuatiliwa zaidi kwa upande wa Yanga. Bila shaka atakuwa katika presha ya kuthibitisha ubora uliokuwa ukitajwa kutoka kwake. Ni mchezaji aliyetoka ligi ya pili kwa ukubwa nchini Brazil hivyo anaweza kucheza vile alivyozea ili kuisaidia timu yake kupata ushindi.

Danny Mrwanda


Katika michezo mitatu ya mwisho baina ya mahasimu hao, Mkude ameonekana kumuweza Niyonzima kwa kumzuia kuichezesha timu yake kwa kwenda mbele. Niyonzima amekuwa akifichwa na kiungo wa Taifa Stars ambaye huhakikisha hampi nafasi mpinzani wake kusonga mbele na mipira huku akitengeneza pasi za mwisho kwa washambuaji wake. Licha ya kuonekana kumthibiti Niyonima katika michezo miwili iliyopita, bado mchezesha timu huyo atakuwa mchezaji watatu wa kuchungwa zaidi na Simba kwa muda wote atakaokuwepo uwanjani.

Pierre Kwizera anaweza kuanza sambamba na Ndemla na Mkude katika safu ya kiungo ya Simba, na watatu hao ni wachezaji wanaokaba kwa umakini huku pia wote wakiwa ni wachezesha timu hodari. Kwizera ni mzuri katika kuanzisha mashambulizi na kupiga pasi katika njia sahihi kwa safu ya mashambulizi, Ndemla ni atakuwa mchezaji hatari zaidi katika eneo la kiungo la Simba kutokana na uwezo wake wa ziada katika kupiga pasi za ‘ kupenyeza’ hata akiwa katika umbali mrefu.

Kwa kasi ya Okwi na Sserunkuma na ujanja wa Tambwe makosa mawili tu katika safu ya ulinzi ya Yanga yatawamaliza na kuharibu mipango yao yote. Simba wana tatizo la kuchoka mapema, Yanga ni timu inayocheza kwa nguvu muda wote lakini kiwango cha Emerson ndicho kitakachowapa nafasi ya kushinda.

NI OWINO SQUARE? v WAGUMU, NADIR NA KELVIN…

Dan Sserunkuma

Mlinzi wa timu ya Taifa ya Kenya, Hambee Stars, David Owino anaweza kuanza mahala kwa Hassan Isihaka na kucheza na nahodha, Joseph Owino. Kama Phiri anaanza
Na ‘ Owino-Square’ mechi itakuwa ngumu sana kwa Yanga hata kama mshambulizi mpya, Mliberia, Kpah Sherman ataanza na Mrwanda. William Lucian ataanza katika nafasi ya beki mbili wakati Mohammed Husein atanza katika beki-tatu, hakutakuwa na kasi ya kutisha kutoka kwa wachezaji wa Yanga, lakini makosa machache tu yanaweza kuwapatia ‘ credit’ Ngassa na Msuva.

Mbuyu na Oscar Joshua wnataraji kuanza katika safu ya ulinzi wa pembeni kwa upande wa Yanga, Yanga itakuwa ngumu kupitika sehemu za pembeni. Nahodha, Nadir Haroub na Kelvin Yondan wataanza katika safu ya kati-beki 4 na 5, na wawili hao wamekuwa bora kwa mwaka wote. Wataweza kuwazima washambuliaji wenye uchu wa Simba?. Simba watafunga katika mchezo huu na ubora w walinzi hao utaonekana baada ya dakika 90. Nani mshindi wa mchezo huu?

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA