PHIRI ASEMASIMBA SASA IMEIVA, ANAYEKATIZA MBELE HALALI YAO

Baada ya kuichapa Yanga mabao 2-0 na kufanikiwa kunasa saini za nyota watatu wapya kutoka Uganda, kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri alisema kikosi chake sasa kimeiva na anaamini kitafanya kazi nzuri msimu huu.

Simba iliinyanyasa bila huruma Yanga kwa kuipa kipigo cha pili katika mechi ya Nani Mtani Jembe 2 iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Katika mechi hiyo, Simba iliwatumia wachezaji wawili kutoka Uganda waliokuwa wametua nchini kwa ajili ya kufanya majaribio, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Simon Sserunkuma kabla ya juzi kuwasanisha mikataba baada ya kuridhika na viwango vyao.

Katika mahojiano na NIPASHE jijini jana, Phiri alisema kikosi chake kimeimarika na kinampa matumaini ya kufanya vizuri katika mechi zinazofuata za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu baada ya kuanza vibaya katika mechi sita za awali walizoambulia sare.

"Kesho (leo) tutaanika wachezaji wote walioingia na kutoka Simba kabla ya timu yetu kuingia kambini Ndege Beach (Dar es Salaam) mwishoni mwa wiki kujiandaa kwa VPL.


"Nisingependa kuongelea kuachwa kwa (Amissi) Tambwe na (Pierre) Kwizera kwa sababu muda wa usajili haujafungwa na suala hilo litaelezwa na uongozi kesho (leo).

"Kikubwa nilikuwa ninasaka muunganiko mzuri wa timu ambao sasa umeanza kuoneakana. Tumekuwa na mwanzo mbaya katika ligi ndiyo maana tumelazimika kufumua kikosi kwa kiasi kikubwa," alisema Phiri.

UHURU AVUNJA MKATABA

Katika hatua nyingine, kiungo mshambuliaji wa klabu ya hiyo Uhuru Seleman ameweka wazi kuwa ombi lake kuitaka Simba ivunje mkataba wake limekubaliwa.

"Nilituma barua ya kuomba klabu isitishe mkataba wangu bila malipo ili niweze kuwa huru kutafuta timu nyingine ya kuchezea, ninashukuru sana uongozi wa Simba umelikubali ombi langu. Sasa nipo huru," alisema Uhuru jijini jana.

Alisema anatarajia kujiunga na Mwadui FC ya mkoani Shinyanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) ili kuboresha kiwango chake kabla ya kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kujiunga na Klabu ya Jomo Cosmos.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA