TAIFA STARS INAPOKUWA MDOGO MBELE YA YANGA NA SIMBA
Na Prince Hoza Matua
NASHANGAA sana pale ninaposikia sakata la vilabu vikubwa vya Simba na Yanga dhidi ya TFF na hasa timu ya taifa, Taifa Stars nashindwa kuelewa, ni ukubwa wa vilabu hivyo kwa TFF ni nguvu kubwa walizonazo toka kwa mashabiki wake.
Shirikisho la soka nchini, TFF linaloongozwa na Wallace Karia, limekuwa mdogo mbele ya Yanga na hata Simba pia, huwaga sipati picha ninapoona kiongozi ama viongozi wa Yanga anapokuwa na nguvu ya kimaamuzi dhidi ya TFF.
Kabla sijaingia kwenye mada yangu ya leo ambayo imenilazimu kuwataja TFF na Yanga pamoja na Simba, ni kwa sababu ya jambo lililo mbele yetu katika upande wa soka kuwahusu wao zaidi.
Wiki hii na ijayo timu yetu ya taifa, Taifa Stars itakuwa na michezo miwili ya kufuzu AFCON ya 2027 itakayofanyika hapa nchini, Tanzania itakuwa mwenyeji wa AFCON lakini ikishirikiana na Kenya na Uganda.
Licha ya uenyeji wake, lakini inatakiwa kushiriki ngazi ya awali, ikitakiwa kufuzu ambapo Stars itakuwa na mechi mbili mfululizo za kufuzu, kwa maana hiyo kocha wa timu hiyo Miguel Angel Gamondi ameteua kikosi chake kwa ajili ya kukaa kambini Ili kujaribu bahati yake tena.
Katika kikosi alichoita wapo baadhi ya wachezaji kutoka timu mbalimbali za hapa nchini na wengine ughaibuni Ili kutengeneza muunganiko wa kutengeneza Taifa Stars, wachezaji wanaotoka Simba na Yanga ni tegemeo sana.
Na hata klabu ya Yanga na hata Simba zinatambua umuhimu wao kuunda timu ya taifa, zamani mchezaji akiitwa kutoka Simba au Yanga hujisikia furaha sana, kwa sababu timu ya taifa inamuongozea nguvu kubwa na ushawishi kwake kimaendeleo.
Ila sasa kumezuka tabia mbaya kwa Yanga na Simba kuhusu kuwang' ang' ania wachezaji wake, na pengine viongozi wa timu hizo wakizuia wachezaji wao wasijiunge na timu ya taifa.
Hivi karibuni vilabu vyote viwili, Simba na Yanga kwa pamoja viliungana na kutoa wachezaji wake kwenye kambi ya timu hiyo iliyokuwepo nchini Morocco, Taifa Stars ikiwa Morocco ikijiandaa kucheza mechi za majaribio, vilabu vya Yanga na Simba viliwachomoa wachezaji wake Ili kuja kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu iliyowahusu wao wenyewe.
Kocha wa timu hiyo Miguel Gamondi alilalamika sana lakini hakuna aliyeelewa somo hilo, na wala Shirikisho la soka nchini, TFF lilikaa kimya, najua viongozi wa TFF ni wadogo mbele ya Yanga na Simba.
Tatizo hilo limejirudia tena na hasa kwa Yanga ikiwazuia wachezaji wake Dickson Job na Clement Mzize kwa madai kwamba ni majeruhi, kiukweli Mzize na Job si majeruhi na wapo fit lakini Yanga ipo juu ya TFF.
Madai ya Yanga kwamba wachezaji wake hao ni majeruhi, SI kweli kwa sababu wameanza kucheza mechi za mashindano na sasa wanafanya mazoezi na timu hiyo huko Zanzibar.
Yanga ilisafiri hadi Zanzibar na miongoni mwa wachezaji iliwao nao ni wawili hao, Mzize na Job walijumuhishwa na Gamondi kujiunga na timu hiyo ila baadaye viongozi wa Yanga walikuja juu wakipingwa kuitwa kwao.
Hii ni tabia mbaya ya klabu kukataa mchezaji wake ama wachezaji wake kuitwa timu ya taifa, mchezaji kuitwa timu ya taifa ni lazima kujiunga na wenzake, wito wa mchezaji kwenda timu ya taifa ni sawa na raia mwema kuitwa jeshimi kwa ajili ya kambi ya kwenda kupigania taifa.
TFF iweke sheria kwa klabu bila kujali Yanga au Simba mchezaji wake anapoitwa Stars na asipojiynnga nayo adhabu kali itolewe kwa klabu husika na ikiwezekana timu yenyewe ipokwe pointi ama kutozwa faini kidogo itakuwa na maana sana.
Sidhani kama Dickson Job ama Clement Mzize wenyewe wanafurahia hilo ila klabu yake inachukua hatua kwa sababu TFF Iko chini yao, ikumbukwe Yanga imewahi kuwaambia TFF kwamba haiwataki viongozi fulani wa Bodi ya Ligi na kweli viongozi hao wakaondolewa.
ALAMSIKI
