Mangungu awataka Wanasimba kuwa wamoja
Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amewataka Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo kudumisha utulivu wakati huu ambao klabu inaelekea katika mchakato wa uchaguzi, akisisitiza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa mujibu wa Katiba na taratibu zilizowekwa.
Mangungu amesema licha ya kuwepo kwa changamoto na misuguano mbalimbali ndani ya klabu hiyo, amejitahidi kusimamia mambo kwa kuzingatia taratibu na kuhakikisha kuwa tofauti zilizojitokeza hazisababishi mpasuko mkubwa ambao ungeweza kuleta hasara kwa klabu.
Kuhusu suala la uchaguzi, Mangungu ameeleza kuwa kwa mujibu wa utaratibu uliopo, uchaguzi hufanyika baada ya muda wa uongozi uliopo kukamilika, huku akibainisha kuwa muda wa mwisho wa uongozi wa sasa ni Januari 30, ambapo miaka minne ya uongozi itakuwa imetimia.
Aidha, amewataka Wanachama wenye hoja au maoni kuhusu mchakato huo kuyawasilisha kupitia vikao vinavyotambulika badala ya kutumia misukumo inayoweza kuathiri utulivu na mshikamano wa klabu.
