Lameck Lawi aomba kuondoka Azam
Beki wa kati wa Azam FC Lameck Lawi ameandika barua ya kuomba kuondoka Azam FC katika dirisha dogo la usajili linalokuja ili ahamie timu nyingine ambapo atapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza baada ya kukosa nafasi hiyo Azam FC.
Lawi alijiunga na Azam FC akitokea Coastal Union na hana nafasi chini ya kocha Florent Ibenge ambaye nae ni kama bado hana kikosi maalum cha kwanza kutokana na mabadililo ya mara kwa mara.
“Ni kweli Lawi ameomba kuondoka dirisha dogo anataka kwenda kutafuta changamoto nyingine nje ya Azam FC ambayo kwa sasa anapata nafasi ya kufanya mazoezi na timu bila ya kucheza.” kimesema chanzo cha uhakika ambacho hakijataka jina lake litajwe.
Mara ya mwisho Lawi kuitumikia Azam FC kwenye mechi za ushindani ilikua Mapinduzi Cup Zanzibar dhidi ya Simba SC, Lawi aliifungia timu yake bao la kichwa dakika ya 73 kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi mnamo Januari 8, 2026 lakini pia alionekana dhidi ya Yanga kwenye CRDB Cup.
