Mechi itakuwa ngumu- Steve Barker
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amezungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao Yanga SC, ambapo Simba watakuwa wenyeji. Barker amebainisha mikakati na mbinu atakazotumia kupambana na wapinzani wao katika mchezo huo mgumu.
Barker amekiri kuwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu unakutanisha vikosi viwili bora zaidi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kocha huyo amebainisha kuwa Yanga wako imara sana maeneo ya pembeni kupitia mawinga wao na walinzi wa pembeni kama Chadrack Boka na Mohamed Hussein, ambao wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi na ndiko walikopatia goli lililowapa ushindi katika mchezo uliopita. Amesisitiza kuwa wamejiandaa vyema kukabiliana na hatari hiyo.
Barker amekiri kuwa eneo lake la kiungo limekuwa na makosa madogo madogo, lakini wachezaji wote wanajua nini kinatakiwa kufanyika ili kufanya vitu sahihi na kupunguza makosa uwanjani.
Kocha huyo ametahadharisha kuwa ingawa Yanga wanapenda kuweka presha kubwa, Simba pia wataenda kuwashambulia kwa presha kubwa na ana mashaka kama Yanga wataweza kumudu presha hiyo watakayopelekewa.
