Katibu wa wizara ya utamaduni ashiriki ujenzi wa uwanja wa AFCON, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Oktoba 24, 2026 ameshiriki kazi za umwagaji wa zege na uwekaji wa majukwaa ya uwanja mpya wa michezo wa Dodoma unaojengwa katika eneo la Nzuguni jijini humo.

Ujenzi wa uwanja wa Dodoma umefikia asilimia 20 ambapo kwa sasa unafanyika ufyatuaji wa teknolojia wa majukwaa na kupachika (precast) ambayo inasaidia kwenda haraka na kuwa bora zaidi.

Uwanja wa Dodoma utakuwa na uweza wa kuchukua watazamaji 33,300 na umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2027.

Msigwa ameeleza kufurahishwa na kasi ya ujenzi ya mkandarasi Limonta SPA wa Italia na Mshauri Elekezi Dar Alhandasah wa Misri na amewataka waendelee kuongeza kasi ili kufidia muda uliopotea wakati wa majadiliano ya usanifi wa kabla ya kuanza kwa kazi za ujenzi.

Amewapongeza vijana wa Kitanzania wanaofanya kazi katika mradi huo wakiwemo mafundi na wahandisi ambao kwa idadi ni zaidi ya asilimia 90 na amewahakikishia katika mradi huo sio tu watapata kipato bali watavuna ujuzi ambao utawawezesha kutekeleza miradi mikubwa kama huo bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.

Uwanja Dodoma ukikamilika utaiwezesha Tanzania kuwa na jumla ya viwanja 7 vyenye sifa ya kutumika katika mashindano ya Kimataifa vikiwa na uwezo wa daraja la 3 na 4 (CAF Category 3&4) na hivyo kuiwezesha Tanzania kukidhi vigezo vya kuwa mwenyeji pekee wa mashindano makubwa ya Afrika (AFCON).

Viwanja hivyo ni Benjamin Mkapa na Uhuru (Dar es Salaam), Uwanja wa Arusha, Uwanja wa Dodoma, Uwanja wa Amani (Zanzibar), Fumba (Zanzibar) na Kizimkazi (Zanzibar)






Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons