Baada ya kushindwa kufuzu, Vipers yatimua kocha
Uongozi wa Vipers SC umemfuta kazi kocha Denis Lavagne, baada ya mabingwa hao wa Uganda kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Vipers SC imetolewa kwenye michuano hiyo kwa matokeo ya jumla ya raundi ya kwanza hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Nouadhibou ya Mauritania, ambapo katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa nyumbani (St. Mary's Stadium, Kitende) timu hizo zilitoka sare ya 1-1, na mchezo wa mkondo wa pili ugenini ulimalizika kwa sare ya 0-0.
Kutokana na matokeo hayo, FC Nouadhibou imesonga mbele kwa faida ya goli la ugenini.
Kocha huyo raia wa Ufaransa amesitishiwa mkataba wake ikiwa ni miezi michache tu tangu aajiriwe mwezi Juni mwaka huu.
Sababu nyingine inayotajwa kuchangia uamuzi huo ni mwenendo usioridhisha wa timu hiyo kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Uganda, ambapo kwa sasa inashika nafasi ya tano ikiwa na alama 11 baada ya kucheza michezo sita.
