Yanga SC wafanya semina ya usalama wa watoto
Leo tumefanya semina kwa vijana ikihusisha mada mbalimbali muhimu, ikiwemo usalama na ulinzi wa watoto (Safeguarding & Child Protection), uzoefu wa safari za kimataifa pamoja na maarifa na misingi ya ufundishaji wa soka kwa vijana.
Kupitia makubaliano yetu na Dulla Sports Centre ya Zanzibar katika kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana, moja ya maeneo muhimu tuliyokubaliana ni kubadilishana uzoefu, maarifa na utaalamu kwa lengo la kuwajengea vijana mazingira bora ya kukuza vipaji vyao ndani na nje ya uwanja.
Tunaamini uwekezaji katika maarifa, malezi na maendeleo ya vijana ni sehemu muhimu ya kujenga kizazi cha wachezaji wenye uwezo, nidhamu na uelewa mpana wa soka.
