Yanga hawana presha na Geita Gold kesho

Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema hana presha kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Geita Gold, akisema yuko kwenye nafasi ambayo alitamani kuwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo utakaochezwa kesho, Septemba 15, 2026, Manqoba amesema Yanga inapaswa kufurahia ushindani na kuchukua mchezo mmoja baada ya mwingine, huku akisifu uwezo wa Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila.

“Sina presha, niko kwenye nafasi ambayo nilitamani kuwa. Tunapaswa kufurahia ushindani na kuona mapambano yataishia wapi. Hii ni ligi yenye ushindani mkubwa na bado hatujacheza dhidi ya baadhi ya timu kubwa, hivyo tunapaswa kuchukua mchezo mmoja baada ya mwingine,” amesema Manqoba.

Amesema Geita Gold ni timu yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa kiufundi, mpangilio mzuri, ulinzi ulioshikamana na uwezo wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza, hivyo wanafahamu kuwa hawatacheza dhidi ya wapinzani wepesi.

“Tunakwenda kukutana na timu nzuri sana. Ina wachezaji wenye uwezo mkubwa kiufundi, ni timu yenye mpangilio mzuri, iliyoshikamana kwenye ulinzi na yenye uwezo mkubwa wa kufanya mashambulizi ya kushtukiza. Ni timu ambayo inaweza kushangaza na kuifunga timu yoyote, hivyo tunafahamu hatuchezi dhidi ya wapinzani wepesi,” amesema Manqoba

Kwa upande wake, beki wa Yanga, Mohamed Hussein, amesema wameitazama Geita Gold na kubaini ubora pamoja na mapungufu yao, ambayo watafanyia kazi kuelekea mchezo huo.

“Kama timu tunaendelea vizuri kwa ajili ya mchezo wa kesho. Ni kweli hatukuwa na muda mrefu wa kufanya maandalizi makubwa, lakini tunaamini maandalizi ya jana na leo yatatusaidia kuwa tayari kwa mchezo,” amesema Mohamed Hussein.

Yanga itashuka dimbani dhidi ya Geita Gold kesho, Septemba 15, 2026, saa 1 usiku.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Kocha Simba anataka wachezaji wapya watano

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI