Waandaaji miaka 30 ya bongofleva wamlipia faini Dudubaya
Waandaaji wa Tamasha la Miaka 30 ya BongoFleva wametangaza kutekeleza adhabu iliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kumlipia kiasi cha shilingi milioni tatu Msanii Godfrey Tumaini maarufu kama Dudu Baya.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Mmoja wa Waratibu wa Tamasha hilo, Madee Ali amesema baada ya kupokea maamuzi ya BASATA, wamekubali kuyatekeleza na kwa haraka kulipa faini iliyotolewa kwao, pamoja na kulipa faini iliyotolewa kwa Msanii Dudu Baya.
Waandaaji hao wameihakikishia BASATA pamoja na Wadau wa sanaa Nchini kuwa wanaheshimu maamuzi yaliyotolewa na wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taratibu na Sheria zilizowekwa.
Aidha, wameeleza kuwa ushirikiano, uwajibikaji na uzingatiaji wa Sheria ni miongoni mwa misingi muhimu katika kulinda, kukuza na kuendeleza sekta ya sanaa Nchini.
“Tunatoa shukrani kwa BASATA na Wadau wote kwa ushirikiano wao, huku tukiahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha Sekta ya Sanaa inakua na kuendelezwa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kitaaluma,”
