Sowah afunguka ishu ya kuchana picha ya Injinia Hersi

Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Jonathan Sowah, amefunguka kuhusu tukio la kuchana picha ya Rais wa Young Africans (Yanga SC), Eng. Hersi Said, katika video ya utambulisho wake baada ya kujiunga na klabu hiyo kutoka Kariakoo.

Sowah, raia wa Ghana, amesema kitendo hicho hakikuwa uamuzi wake binafsi, bali kilikuwa sehemu ya maudhui na maelekezo aliyopewa na klabu kwa ajili ya utambulisho wake kwa mashabiki.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Sowah amekiri kuwa wakati mwingine hukumbuka tukio hilo na kujisikia vibaya, akieleza kuwa katika mazingira yale hakuwa na nafasi ya kukataa kutokana na kuwa mchezaji mpya aliyekuwa amejiunga na klabu hiyo kwa ajili ya kucheza soka na kutafuta kipato.

“Kuna wakati huwa najisikia vibaya. Kile kilichotokea sikuwa na namna wala sikuwa na chaguo lolote. Nilikuja huku kutafuta pesa, nilipaswa kufanya kile wanachotaka nifanye,” alisema Sowah.

Tukio hilo lililenga kuongeza msisimko na kuibua ushindani wa jadi kati ya Simba na Yanga, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukitawaliwa na utani na matukio mbalimbali nje na ndani ya uwanja.

Hata hivyo, kitendo hicho kilizua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka nchini, huku baadhi wakikiona kama sehemu ya burudani na utambulisho wa mchezaji, na wengine wakikosoa namna kilivyowasilishwa.

Kauli ya Sowah sasa imeongeza sura nyingine katika mjadala huo, huku akieleza kuwa kama mchezaji mpya, aliona ni wajibu wake kutekeleza maudhui aliyotakiwa kufanya na klabu yake wakati wa utambulisho.

Kauli hiyo pia inaibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya wachezaji wa kigeni katika maudhui ya kimasoko na ushindani wa klabu, hasa wanapowasili katika ligi zenye ushindani mkubwa na upinzani wa jadi kama ilivyo kwa Simba na Yanga.


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Kocha Simba anataka wachezaji wapya watano

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI