Mkude afunguka kuhusu maisha yake
Kiungo mzoefu wa mpira wa miguu nchini, Jonas Mkude, amefunguka kuhusu maisha yake ya utotoni na mwanzo wa safari yake ya soka, akibainisha kuwa mama yake mzazi hakiamini kama mchezo huo ungekuwa na mchango wowote katika maisha yake ya baadaye.
Akizungumza hivi karibuni alipokuwa mgeni katika Podcast ya Denis Nkane kwenye kipindi cha Physics, Mkude alieleza kuwa alilelewa akiwa mtoto wa pekee kwa mama yake, hali iliyofanya mama huyo kuweka msisitizo mkubwa zaidi kwenye masomo yake ya darasani kulikoo michezo.
Hata hivyo, mwelekeo wa maisha yake ya soka uliokolezwa na mjomba wake, Peter Toshi, ambaye alichukua jukumu la kumshawishi mama yake ili amruhuse kijana huyo kuanza mazoezi ya mpira wa miguu katika maeneo ya ufukweni.
"Mimi ni mtoto wa pekee kwa mama yangu. Mama alitilia mkazo sana elimu na hakuwa akiamini kabisa kama mpira ungetengeneza maisha yangu. Lakini mjomba wangu, Peter Toshi, ndiye aliyemshawishi mama na kuanza kunichukua kwenda kufanya mazoezi ya soka bichi." — Jonas Mkude.
