Beki Simba asimulia maisha yake ya mtaani
Beki wa timu ya Simba SC, Rushine De Reuck, amefunguka kuhusu mazingira magumu na hatarishi aliyokulia wakati wa mahojiano yake katika kipindi cha Micro Moments of Self-Love kinachoongozwa na Fatema Dewji.
Mchezaji huyo alieleza kuwa alizaliwa na kukulia katika eneo la Kensington lililopo mjini Cape Town, Afrika Kusini.
Eneo hilo linasifika kwa kuwa na mazingira yanayotawaliwa na umasikini, matukio ya mauaji, pamoja na ushawishi mkubwa wa magenge ya wahalifu au gangsterism.
Katika kuangazia changamoto za kifamilia na kijamii zilizomzunguka, De Reuck alibainisha jinsi hatari hiyo ilivyokuwa karibu na maisha yake ya kila siku kiasi cha kuathiri familia yake ya karibu.
Akieleza hali hiyo, alibainisha: "Baba yangu na kaka yangu mkubwa walikuwa wakijihusisha na mambo ya magenge". Aliongeza kuwa wengi wa marafiki zake wa utotoni pia walitumbukia kwenye mkumbo huo wa magenge, ambapo wengi wao walipoteza maisha na wengine wapo gerezani wakitumikia vifungo.
Licha ya kuzungukwa na vishawishi hivyo pamoja na mazingira yaliyowavuta wengi kwenye uhalifu na mauti, De Reuck alifanikiwa kujinasua na kutumia mpira wa miguu kama fursa ya kubadilisha maisha yake. Akirejelea ukweli wa mazingira aliyoyavuka, alieleza:
"Eneo hilo linajulikana sana kwa kuwa na ushawishi mkubwa wa magenge ya wahalifu, umasikini, matukio ya mauaji, na uhalifu", akionyesha jinsi safari yake ya michezo ilivyomwezesha kuepuka hatima mbaya iliyowakuta vijana wengi
