ONANA ASEMA HUU NDIO MWAKA WA SIMBA KUTINGA NUSU FAINALI
Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon na Simba SC, Willy Onana, amesema huu ndiyo wakati muhimu kwa timu yake kwenda kuandika historia mpya Barani Afrika kwa kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mara ya kwanza.
“Binafsi najisikia vizuri kucheza Robo Fainali kwa mara ya kwanza, Al Ahly ni kama Real Madrid kwa Afrika inaweza kuwa katika kipindi cha mpito lakini katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wanakuja kivingine.
Tunatambua tunakwenda kucheza na timu kubwa sana barani Afrika, hizi ni nyakati bora kwa wachezaji na viongozi wa Benchi la Ufundi kuandika historia mpya,”
Amesema kama kuna aliyekuwa akiingalia Simba SC ikiishia hatua ya Robo Fainali abadilishe mtazamo kwa kuwa huu ni wakati wa kwenda kubadili hii historia ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakiisubiri.
“Sijui mipango ya mwalimu katika mchezo huo lakini mimi binafsi niko tayari kwa ajili ya mechi hii kubwa ambayo itatazamwa na watu wengi Barani Afrika,” amesema Onana.
Simba SC imefika hatua hiyo baada ya kuishia nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi B kwa alama tisa nyuma ya Asec Mimosas ya Ivory Coast ikiwa na alama 12.