SINGIDA UNITED YAENDELEA KUIBOMOA TANZANIA PRISONS, YAMNASA KIUNGO NYOTA
Na Saida Salum. Dar es Salaam
Matajiri wa kulima Alizeti, timu ya Singida United leo tena imemtambulisha kiungo mshambuliaji Eliuta Herman Mpepo na kumtangaza rasmi kuwa mchezaji wake baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili.
Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga amemtambulisha mchezaji huyo ambaye alikuwa moto wa kuotea mbali katika kikosi cha Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya, lakini anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa akitokea kwa maafande hao wa jeshi la Magereza.
Mara ya kwanza Singida United ilimtambulisha kiungo Kazungu Mashauri ambaye naye alisaini miaka miwili, Sanga amesema usajili wa Mpepo ni sehemu ya kukiimarisha kikosi chao ambacho msimu ujao kitakuwa chini ya Hemed Morocco aliyechukua mikoba ya Mholanzi Hans Van der Pluijm aliyehamia Azam Fc.
Tayari wana fainali hao wa kombe la TFF maarufu Azam Sports Federation wameshakamilisha usajili wa nyota wengine sita ambao ni Danny Lyanga, Tibar John, Felipe Dos Santos, Amarra Diaby, Habibu Kiyombo na Mashauri