BOCCO AWA MWANASOKA BORA WA MWEZI JANUARI, VPL
Na Prince Hoza. Dar es Salaam
Nahodha na mshambuliaji wa vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba Sc, John Raphael Bocco "Adebayor" ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Bocco ameshinda tuzo hiyo baada ya kufanikiwa kuwashinda Emmanuel Okwi pia wa Simba na Awesu Awesu wa Mwadui Fc, mshambuliaji amefanya vizuri katika mwezi Januari na kuisaidia timu yake kushinda mechi tatu akishiriki kikamilifu kwa mechi zote.
Kwa mujibu wa kamati ya tuzo kwa kushirikiana na makocha, wamejiridhisha kumpa Bocco tuzo hiyo hasa baada ya kuimarika kwa kiwango, hadi sasa Bocco amefunga jumla ya mabao tisa akishikilia nafasi ya tatu.
Tuzo hiyo msimu huu ilianza kwenda kwa Mganda Emmanuel Okwi aliyeshinda Agosti, Septemba ilienda kwa Shafik Batambuze naye ni Mganda wakati Oktoba ilienda kwa Mzambia Obrey Chirwa.
Wengine walioshinda tuzo hiyo ni Mudathir Yahya mwezi Novemba na Habibu Kiyombo aliyeshinda mwezi Desemba, Bocco sasa atajinyakulia kisumbuzi kutoka Azam pamoja na kitita cha shilingi Milioni moja.