STAA WETU
SHOMARI KAPOMBE. AMERUDI KUWASHIKA.
Na Prince Hoza
MCHEZAJI ambaye sikutaka asajiliwe na Simba msimu huu ni Shomari Kapombe, kitu pekee kilichonifanya nisipende asajiliwe ni majeruhi aliyonayo ambayo nilidhani kama yatamfanya asirejee katika ubora wake.
Ama kweli nililaani sana usajili wa Kapombe mpaka kufikia kumshutumu mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Kapteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). Zacharia Hanspoppe, sikuona mantiki yoyote Simba kumuacha Mkongoman Janviel Bokungu na kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo pia wa kucheza kama beki.
Kapombe ni mchezaji mzuri na ndio maana akapata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Ufaransa katika klabu ya Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la nne.
Lakini tatizo kubwa linalomsumbua maishani mwake ni maumivu ya nyonga, inafikia wakati Kapombe anatamani kuachana na soka na kufanya shughuri nyingine, Kapombe amekosa raha kwa kipindi kirefu hasa akiwa nje ya uwanja akiuguza majeraha yake.
Nyota huyo alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Azam Fc na tangu alipotua Simba hakuwa na mwanzo mzuri kwani alishindwa kuitumikia klabu yake baada ya kutonesha jeraha lake akiwa kwenye mazoezi ya timu ya taifa, Taifa Stars.
Kapombe aliumia mazoezini wakati Stars ikijiandaa kushiriki michuano ya COSAFA CASTLE CUP iliyofanyika nchini Afrika Kusini, baada ya kuumia, Kapombe alikuwa akipatiwa matibabu yaliyomweka nje kwa kipindi cha miezi mitano.
Alikosa mechi 12 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, michuano ya FA na kombe la Mapinduzi na pia alikosa mechi ya kuwania Ngao ya Jamii na zile za maandalizi ya msimu, kwa bahati nzuri beki huyo amerejea uwanjani na nwanzoni mwa wiki hii aliichezea Simba kwa mara ya kwanza ilipoumana na Kagera Sugar, mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Kapombe aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Mghana, Nicolaus Gyan na kuweza kuonyesha kwamba yeye bado ni mchezaji bora isipokuwa majeraha tu ndio yaliyokuwa yakimtesa, mchezo huo uliofanyika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Simba ilishinda mabao 2-0.
Kapombe alihusika kuseti bao la pili baada ya kuingia nao mpira hadi karibu ya lango la Kagera Sugar na kumpasia nahodha John Raphael Bocco "Adebayor" aliyeuweka kimiani na kumuacha kipa mkongwe Juma Kaseja asijue la kufanya na kuwa bao la pili huku goli la kwanza likifungwa na kiungo Said Ndemla.
Kapombe alikaribia kuseti lingine lakini Emmanuel Okwi alichelewa, huyo ndiyo Shomari Salum Kapombe aliyezaliwa mjini Morogoro Januari 28, 1992 na kuanza kuonyesha kipaji chake katika timu ya Morogoro Youth Academiya kabla ya kujiunga na Polisi Moro.
Nyota yake ilianza kung' ara alipokuwa kwenye timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 iliyokuwa ikinolewa na Jamuhuri Kihwelo "Julio" ambapo timu hiyo iliweza kutamba katika michuano ya kufuzu mataifa Afrika kwa vijana na ndipo klabu ya Simba ilipoamua kumsajili.
Kapombe alianza kuichezea Simba kuanzia msimu wa 2011 hadi 2013 alipoenda nchini Ufaransa kucheza soka la kulipwa katika timu ya Cannes, alijiunga na timu hiyo msimu wa 2013/14 hakudumu sana akarejea nyumbani Tanzania.
Mwaka huo huo 2014 alijiunga na Azam Fc ambapo alidumu nayo hadi mwaka 2017 aliporejea Simba, Ki- Asilia Kapombe ni kiungo lakini ana uwezo pia wa kucheza karibu nafasi zote uwanjani sijui kipa, na anajulikana kama kiraka.
Katika orodha ya mabeki wanaofunga, sifa ambayo anayo Mghana, Asante Kwasi, Shomari Kapombe naye anayo kwani anasifika kwa kufunga na kutengeneza nafasi ya kufunga, Kapombe amewahi kuwemo katika orodha ya wafungaji bora wakati huo alipokuwa anaichezea Azam Fc.
Kapombe aliingia kwenye mzozo na mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hanspoppe hasa kuhusu kucheza, Hanspoppe alidai beki huyo amepona ila hataki kucheza na akamtaka achague moja kucheza au kuondoka.
Lakini mlinzi huyo alimjibu Hanspoppe kuwa yeye hajapona na hawezi kucheza mpaka atakapopona ila kama Simba wako tayari kumlipa pesa zake basi wavunje mkataba naye, hata hivyo mzozo huo uliishia kwenye vyombo vya habari na mchezaji huyo aliendelea na tiba mpaka kuruhusiwa na daktari wa kkabu ya Simba, Yassin Gembe.
Jumatatu iliyopita Kapombe alidhihirisha ubora wake alipochangia goli ka pili na la ushindi kwa Simba Sc ambao ni vinara wa ligi hiyo kwa pointi 32 huku nyuma yake ipo Azam Fc yenye pointi 30, Kapombe ni kama amerudi kuwashika wale waliokuwa hawamwamini nikiwemo mimi
NAWATAKIA IJUMAA KAREEM, TUKUTANE JUMA LIJALO