STAA WETU:

IBRAHIM CLASS. MTANZANIA WA KWANZA KUTWAA UBINGWA WA NDONDI WA GBC WA DUNIA.
Na Prince Hoza
NAKUMBUKA kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilipata mapokezi makubwa wakati kilipowasili nchini kikitokea Afrika Kusini ambako kilienda kushiriki michuano ya COSAFA Castle Cup.
Taifa Stars ilikamata nafasi ya tatu ambapo ilitunukiwa medali ya shaba na kitita cha fedha, Dola 10,000 za Kimarekani, Stars ililakiwa na waziri wa habari, michezo, sanaa na utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Mwl Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Na pia aliweza kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo akiwapongeza kwa hatua hiyo waliyofikia huku pia akiwataka waongeze bidii na waweze kuishinda Rwanda katika mchezo wao uliofuata wa michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, maarufu CHAN.
Mwakyembe amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu yetu ya taifa inafanya vizuri kwani hiyo si mara yake ya kwanza, alishafanya hivyo mara kadhaa zilizopita wakati alipochaguliwa kuongoza wizara hiyo na mheshimiwa Rais, Dk John Magufuli, aliwahi pia kuhamasisha hivyo kwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Serengeti Boys ambayo ilishiriki fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana wa umri huo nchini Gabon mwaka huu.
Vijana hao wa Serengeti Boys walipokewa kwa halaiki ya viongozi wa kiserikali akiwemo waziri Mwakyembe ambaye ana dhamana kubwa kwenye upande wa michezo, ikimaanisha michezo yote, lakini walimsahau Mtanzania mwingine anayefahamika kwa jina la Ibrahim Class au King Class ambaye naye alitoka kuipeperusha vema bendera ya Tanzania nje ya mipaka yetu.
Ibrahim Class yeye ndiye ameitoa kimasomaso Tanzania naweza kusema kwa mwaka huu 2017 baada ya kufanikiwa kutwaa mkanda wa dunia wa Global Boxing Council (GBC) akimchakaza bondia Jose Ferero wa Panama mchezo ambao ulifanyika nchini Ujerumani na kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa mkanda huo.
Ubingwa wa dunia ni heshima tosha kwa Tanzania lakini bondia huyo anayepigania uzani wa Light Middle Kg 61 hakupata hamasa yoyote kutoka serikalini wala kwenye chama chochote cha ndondi hapa nchini, zaidi ya meneja wake ambaye alimsaidia kumfikisha hapo halipo.
BONDIA IBRAHIM CLASS (KATIKATI) AKIONYESHA MKANDA WAKE.

Class anayenolewa na Habibu Kinyogoli na Rajabu Mhamila maarufu Super D, ana mafanikio makubwa kwenye mchezo huo kwani licha ya kutwaa ubingwa wa dunia wa GBC, Pia anashikilia mkanda wa UBO Afrika ambao aliutwaa baada ya kumchakaza Mtanzania mwenzake Cosmas Cheka.

Ibrahim Class si bondia wa kumbeza kwani ameitoa kimasomaso Tanzania kwani alitwaa mkanda mwingine wa kimataifa wa WPBF kwa kumpiga bondia wa Zambia Mwansa Kabinda kwa TKO, hayo ni mafanikio makubwa kwa mwanamichezo huyo ambaye alipaswa japo kupongezwa na kupewa heshima yake ikiwemo serikali kumpa hamasa kama inavyofanya kwenye soka na riadha.

Ibrahim Class aliyezaliwa miaka 26 iliyopita, ana rekodi ya kucheza mapambano 22 na 18 ameweza kushinda huku manne pekee amepoteza, kitu kikubwa ambacho Class amekisema ni kuhusu yeye kujituma na ndio kumempa mikanda yote hiyo.

Anasema amekuwa akifanya mazoezi ya nguvu kuanzia asubuhi na jioni, pia anammwagia sifa meneja wake kwa kumsaidia na kumfikisha hapo halipo huku akiwaahidi Watanzania kwamba atafikia levo za akina Manny Paquiano au Froiyd Maywether kwani wote hao anawahusudu mno.

Class, mbali na kufanikiwa kuwafikia akina Rashid Matumla "Snake Boy" , Francis Cheka kwa maana ya rekodi zao, lakini amedai amesahaulika sana na anaona kama Tanzania inathamini soka peke yake huku michezo mingine kama ndondi ambayo inaitangaza vema nchi ikiachwa.

Mchezo wa soka umekuwa ukiigharimu nchi fedha nyingi lakini kila kukicha ukizidi kuporomoka, hivi karibuni Shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) ulitoa orodha ya ubora wa viwango kwa timu za taifa, ambapo Tanzania ilianguka kutoka nafasi ya 125 hadi 136

BONDIA IBRAHIM CLASS NA MKANDA WAKE WA GBC

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA