KISPOTI:

SIKUBALIANI NA LIGI KUU KUWA NA TIMU 20 MSIMU UJAO.

Na Prince Hoza

KWANZA kabisa nianze kwa kuupongeza uongozi mpya wa Bodi ya Ligi (TPLB) uliochaguliwa Oktoba 15 mwaka huu, pongezi sana Kaimu mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Andrew Sanga kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi hiyo.

Lakini pia shukrani zangu nyingine nazielekeza kwa makamu mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Shani Christoms Mrigo pamoja na wajumbe waliochaguliwa kuunda kamati ya Bodi hiyo ambayo itakuwa ikisimamia kutoa maamuzi mbalimbali yanayohusu ligi.

Ikumbukwe Bodi ya Ligi inasimamia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL), Ligi Daraja la kwanza Tanzania bara (FDL) na Ligi Daraja la pili Tanzania bara (SDL).

Kupatikana kwa uongozi huo mpya wa Bodi ya Ligi kunakamilisha mchakato mzima wa uchaguzi na pia kunadhihirisha sasa kuwa mambo mapya yanaanza, tayari Shirikisho la mpira wa miguu nchini, (TFF) limeshapata viongozi wake wapya baada ya Jamal Malinzi na wenzake kukamilika kwa kipindi chao cha uongozi.

TFF ilipata Rais wake mpya ndugu Wallace Karia na makamu wake, Michael Wambura, bila shaka viongozi wa TFF na wa Bodi ya Ligi wataweza kushikamana na kuuendeleza mpira wa Tanzania, kitu ambacho ningependa kipewe kipaumbele kwa sasa ni kuiboresha Ligi Daraja la kwanza.

Na kitu kinachonishangaza ni pale niliposikia kwamba msimu ujao Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara itashirikisha jumla ya timu 20, na msimu huu jumla ya timu mbili zitatelemka daraja badala ya tatu kama ilivyozoeleka.

Sipingani hilo isipokuwa sikubaliani na mpango huo kwa maana bado tuna safari ndefu kuelekea huko, Shirikisho letu la mpira wa miguu (TFF) na Bodi yetu ya ligi bado havijaweza kuonyesha ufanisi wao kikazi na inahitaji muda kidogo ili waweze kuaminiana.

Bodi ya Ligi ndio wenye kuendesha na kusimamia Ligi zote tatu ambazo ni kubwa kwa hapa nchini na ndio wenye majukumu ya kupitia mechi zote za mashindano hayo, lakini TFF imekuwa ikiingilia kazi za Bodi ya Ligi kiasi kwamba zimekuwa zikigongana.

Tulijionea msimu uliopita ambapo Shirikisho hilo lilipotengua maamuzi ya kamati ya masaa 72 ambayo ni ya Bodi ya Ligi, hapo utaona jinsi vyombo hivyo vinavyoingiliana, ningefurahi kama TFF ingevunja kamati yake ya mashindano ili kamati hiyo ihamie Bodi ya Ligi kwakuwa wao ndio wenye ligi na TFF ni msimamizi tu.

Nikija na hili la timu 20 kushiriki Ligi Kuu bara msimu naliona gumu na sidhani kama litaenda sambamba na maendeleo ya mpira wetu, tatizo kubwa linalopelekea mimi kuingia wasiwasi ni ratiba yetu ya nchi kwa mashindano yote.

Ligi inayoshirikisha timu 16 inachukua miezi tisa kumalizika, hapo bado hakujafanyika michuano ya Chalenji wala klabu Afrika mashariki na kati, hakujafanyika michuano ya kombe la Mapinduzi ambayo nayo husimamisha ligi, bado mashindano kama ABCBank ambayo yalifanyika mara moja tu hajafanyika tena.

Ratiba yetu itakuja kuumbua hili la timu 20 ambayo sasa nahisi inaweza kuchezwa mwaka mzima, TFF kama eangejikita kutengeneza vizuri mfumo wa soka letu halafu Bodi ya Ligi ikacheza na kalenda ili masuala ya kuhairisha mechi ama kusogeza mbele mechi isingekuwepo.

Hakuna haja kusogeza mbele mechi za ligi kama kalenda ya FIFA, tunayo, kalenda ya CAF tunayo, kalenda ya CECAFA tunayo nadhani hapo kungesaidia kupanga rariba nzuri za ligi zetu ambazo hazitaingiliana na kalenda za mashirika hayo makubwa ya mpira.

Tatizo tulilonalo Watanzania kujifanya tunajua wakati hatujui, tumekuwa wanafikiwanafiki, hatuwezi kusimamia ukweli, na ndio maana tumekuwq tukikubali kila tunachoambiwa na bwana mkubwa, kulikuwa hakuna umuhimu wowote wa kukubali timu 20 zicheze Ligi Kuu msimu ujao.

Ligi Daraja la kwanza ndiyo iliyohitaji maboresho, haiwezekani ikaitwa Ligi Daraja la kwanza halafu ikachezwa kwa makundi, hilo nalo ni tatizo, haiwezekani hadhi iliyonayo Ligi Daraja la kwanza ikachezwa bila kuwepo mdhamini ambaye angezisaidia timu hizo kusafiri eneo moja kwenda lingine kushiriki ligi hiyo.

Maboresho Ligi Daraja la kwanza yakifanikiwa kwa asilimia 70 hapo sasa uwezekano wa kuongeza timu Ligi Kuu bara ungefanyika, lakini pia bado tunahitaji mabadiliko zaidi kwenye uendeshaji wa Ligi Kuu na tatizo hilo tungetaka lisijirudie.

Haiwezekani Ligi Kuu isimame wiki nzima kupisha timu ya taifa icheze mchezo wa kirafiki, ilipaswa ligi ichezwe angalau katikati ya wiki halafu mwishoni ikacheza timu ya taifa, hili bado tatizo na mnataka kuongeza tatizo, tutaona msimu ujao Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania ikichezwa mwaka mzima.

Tukutane tena Jumatatu ijayo,nawatakia mchezo mwema wa Simba na Yanga Jumamosi ijayo ya Oktoba 28, 2017 ALAMSIKI

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA