Ukata wamwondoa Pluijm Yanga
Na Mrisho Hassan. Dar es Salaam
Ukata unaoiandama Klabu bingwa ya soka Tanzania Bara, Yanga umesababisha mkurugenzi wake wa ufundi Mholanzi Hans Van der Pluijm kuondolewa kwenye nafasi yake hiyo na kutakiwa kurejea zake Uholanzi.
Akizungumza kwa masikitiko kabisa, Pluijm ambaye alikuwa kocha wa Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2014 akichukua mikoba ya Mholanzi mwenzie Ernie Brandts akiinoa kwa nusu msimu kabla ya kutimkia Saudi Arabia.
Pluijm alirejea tena Yanga kama kocha mkuu mwaka 2015 akiipa ubingwa wa Bara mara mbili mfululizo na mataji mengine kama Ngao ya Hisani na kombe la FA, pia akiisaidia Yanga kufuzu nane bora ya kombe la Shirikisho Afrika.
Mwaka jana Pluijm akateuliwa kuwa mkurugenzi wa ufundi huku nafasi yake ikichukuliwa na Mzambia George Lwandamina, ukata ulioanza kuikumba Yanga hasa baada ya kushikiliwa kwa akaunti za mwenyekiti wao Yusuf Manji zimesababisha ukosefu wa kuwalipa mishahara wachezaji wa timu hiyo pamoja na watendaji wengine akiwemo Hans Pluijm.
Katibu mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa amemwambia Pluijm kuwa Yanga haina mshahara wa kumlipa hivyo ni bora akaondoka zake, "Hatukumfukuza kazi, isipokuwa hatuna uwezo wa kumlipa", alisema Mkwasa ambaye aliwahi kuwa msaidizi wa Pluijm mwaka 2014, hali ya kiuchumi inaisumbua Klabu ya Yanga ambayo ilikuwa ikimtegemea Manji ambaye anamatatizo na serikali