KERR ATAMBA KUENDELEZA UBABE MBEYA
Simba ililazimishwa sare na Mbeya City katika mechi zote mbili za msimu wa kwanza (2013/14) wa timu hiyo ya Mbeya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kabla ya kuchezea kichapo katika mechi zote mbili za msimu uliopita wa ligi hiyo, 2-1 nyumbani na 2-0 ugenini, lakini juzi Wanamsimbazi walianza na kikosi chenye viungo watano, Said Ndemla, Jonas Mkude, Abdi Banda, Mwinyi Kazimoto na Justice Majabvi na kuchomoza na ushindi wa 1-0 dhidi ya
timu hiyo mjini hapa.
Kwa safu hii, Simba inaweza kabisa kuondoka na pointi zote sita mbele ya Prisons
Ushindi huo ni mwendelezo wa mabingwa hao mara 18 wa Bara kufanya mabadiliko baada ya mwanzoni mwa msimu kuvunja mwiko wa kugawa pointi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kwa misimu mitatu, safari hii wakichukua pointi sita kutoka kwa African Sports na Mgambo Shooting.
Mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao ya juzi jijini hapa, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola, aliiambia Nipashe kuwa Tanzania Prisons ambao ambayo juzi ilisambaratishwa kwa kipigo kikubwa cha mabao 3-0 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, ijiandae kukumbwa na mabadiliko ya Msimbazi keshokutwa.
"Tumecheza vizuri kipindi cha kwanza, kipindi cha pili hali ya hewa ilitusumbua, lakini muhimu ni pointi tatu kwa sababu uwanja huu (Sokoine) umekuwa mgumu kwetu kwa kipindi kirefu. Tuko hapa Mbeya kwa ajili ya kuvunja mwiko na kupata pointi sita. Tayari tumepata tatu kwa Mbeya City, tunazisubiri pointi tatu nyingine kutoka kwa Prisons Jumatano," alitamba Matola.
Kuhusu mchezaji wa zamani wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' ambaye juzi alicheza kwa mara ya kwanza VPL akiwa na kikosi cha City, Matola alisema: Hakuna asiyejua Boban ni mchezaji mzuri, tatizo linalomsumbua kwa sasa ni kwamba amenenepa, lakini akifanya mazoezi, atawasaidia sana Mbeya City."
Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa Simba, Dylan Kerr, amekiponda kikosi chake kwa kuonyesha kiwango duni kwenye mechi yao ya juzi dhidi ya City.
Katika mahojiano jijini hapa jana, Muingereza huyo alisema: "Sijafurahishwa na namna timu ilivyocheza dhidi ya Mbeya City. Tulizidiwa kwa kiasi kikubwa, goli na ushindi pekee ndicho kitu cha kufurahia hapa, hatukucheza hivi kwenye mazoezi. Mechi haikuwa na furaha kwangu kwa sababu tumecheza soka la Amerika."
Kocha wa Mbeya City, Abdul Mingange, aliliambia gazeti hili jijini hapa juzi kuwa ili timu yake ifanye vizuri VPL msimu huu, watalazimika kusaka washambuliaji wakali wakati wa usajili wa dirisha dogo mwezi ujao.
"Tumetengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini safu yetu ya ushambuliaji imetuangusha. Tunatakiwa kulitumia vyema dirisha dogo kuongeza washambuliaji," alisema meja huyo mstaafu ambaye msimu uliopita alikinoa kikosi cha Ndanda FC ya Masasi, Mtwara.
MECHI ZIJAZO..
Oktoba 21, 2015
Yanga SC Vs Toto Africans
Stand United Vs Majimaji FC
JKT Ruvu Vs Mtibwa Sugar
Prisons Vs Simba SC
Coastal Union Vs Kagera Sugar
Oktoba 22, 2015
Ndanda FC Vs Azam FC
Mwadui FC Vs Mgambo Shooting
Mbeya City Vs African Sports