PLUIJM AKIRI YANGA KUBANWA NA STAND UTD
Licha ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 juzi, kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kuwa wapinzani wao Stand United kutoka Shinyanga waliwazidi uwezo katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Wageni Stand ndiyo walikuwa wa kwanza kuliona lao la Yanga lakini baadaye wenyeji walisawazisha na kuongeza la pili lililodumu hadi mapumziko. Stand walisawazisha mapema kipindi cha pili, kabla ya Yanga kupata penalti iliyowapa ushindi wa 3-2 katika dakika za lalasalama. Akizungumza juzi baada ya mechi hiyo, Pluijm alisema kwamba kikosi chake hakikucheza vizuri, wachezaji hawakuwa na maelewano katika mchezo huo licha ya kushinda.