SIMBA KWENDA Z,BAR LEO, YANGA YAAPA KUTOFUNGWA TENA NA SIMBA

Wakati  timu ya Simba itaenda mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kuanza kambi ya kuwakabili Yanga, mahasimu wao hao wa jadi wamesema timu yao kamwe haitafungwa kizembe tena kama ilivyokuwa katika mechi yao iliyopita.

Yanga ilifungwa kizembe 3-1 dhidi ya Simba katika mechi ya 'Nani Mtani Jembe' kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 21, mwaka jana, mechi ya 'ndondo' iliyowafukuzisha kazi makocha Ernie Brandts raia wa Uholanzi na mzawa Felix Minziro.


Akizungumza jijini hapa mara tu baada ya mechi yao ya raundi ya 25 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara walioshinda 2-1 dhidi ya Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa juzi, kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema hawako tayari kuona tena timu yao inafungwa magoli ya kizembe na Simba katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Simba msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili.

"Tumekosa ubingwa lakini hatuko tayari kufungwa kizembe na Simba katika mechi ya mwisho," alisema Mkwasa.

Naye kocha wa Simba, Mcroatia Zdravko Logarusic alisema jana kuwa anaondoka na wachezaji wote kwa ajili ya kambi hiyo ya mjini Zanzibar.

Loga ambaye ameishuhudia timu yake ikiyumba katika msimu mbaya ambao imefungwa mechi sita na kutoka sare 10 katika mechi zao 25 za msimu huu hadi sasa, amesema atahakikisha anaifunga Yanga ili kumaliza msimu kwa heshima.

Simba iko katika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi hiyo ambayo imeshampata bingwa wake mpya Azam FC aliyeutwaa bila ya kupoteza mechi.

Yanga wamejihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili na ya mwisho ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa na itashiriki Kombe la Shirikisho.

Simba yenye pointi 37 bado haijawa na uhakika wa kumaliza katika nafasi ya nne kwani kipigo Jumamosi na ushindi kwa Ruvu Shooting iliyo chini yake kwa pointi 35 vitawashuhudia Wekundu wa Msimbazi wakimaliza katika nafasi ya tano.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA