DAVID LUHENDE: KUTOKA BEKI HADI USHAMBULIAJI.

Na Prince Hoza

DAVID Luhende kwa sasa anasifika kama kiungo mshambuliaji na amekuwa tishio katika kikosi cha Yanga, kuwepo kwake kumeongeza chachu katika safu ya ushambuliaji na kuifanya timu yake kung'ara.

Mwishoni mwa juma lililopita, Yanga iliibuka na ushindi mnono wa mabao7-0 dhidi ya Komorozine De Dimono ya jamhuri ya watu wa Comoro, ushindi huo mkubwa kwa klabu ya Yanga pengine ni wa kwanza katika uwanja wa Taifa.

Yanga inakuwa timu ya kwanza kuibuka na ushindi mkubwa, timu nyingine iliyopata ushindi mkubwa katika uwanja huo ni Simba SC anbayo iliifunga Mgambo JKT ya Tanga mabao 6-0.

Lakini ushindi wa Simba ulikuwa wa ligi kuu Tanzania bara tofauti na Yanga ambao ushindi wao ni wa michuano mikubwa kuliko yote kwa upande wa vilabu Afrika, yaani ligi ya mabingwa barani Afrika.

Yanga imepata ushindi huo katika mkondo wa kwanza na inatarajia kurudiana nayo mwishoni mwa wiki hii mchezo utakaopigwa huko Moroni mji mkuu wa Comoro.

Endapo Yanga itapata sare ya aina yoyote ile au kufungwa jumla ya mabao 6-0 itakuwa imesonga mbele na itakutana uso kwa uso na mabingwa watetezi wa michuano hiyo mikubwa National Al Ahly ya Misri.

Kama nilivyoanza kumwelezea kijana mdogo, mfupi na mpole awapo nje ya uwanja, David Luhende kwamba amekuwa katika kiwango cha juu baada ya kuhamishiwa mbele badala ya nyuma.


Wakati Yanga ikinolewa na Mholanzi Ernie Brandts, Luhende alikuwa akicheza nafasi ya ulinzi wa pembeni yaani nambari tatu, licha ya kuimudu vema nafasi hiyo na kuwemo katika kikosi cha kwanza cha Yanga, ukuta wa timu hiyo ulionekana kupwaya mno.

Kuna maswali wengi wapenzi wa soka nchini hasa wa Simba na Yanga kwa pamoja walijiuliza inakuwaje ukuta wa Yanga unaoongozwa na mebki bora nchini kama Nadir Haroub 'Cannavaro' na Kelvin Yondani 'Vidic' unaruhusu magoli mengi langoni mwao.

Ukuta huo wa Yanga ulipachikwa majina tofauti huku wengine wakiufananisha na ukuta wa Berlin, lakini ulianza kuwatia wasiwasi mashabiki wao hasa timu yao inaporuhusu magoli ya kizembe.

Lawama nyingi zilielekezwa kwa Cannavaro ambaye ilionekana uwezo wake umeanza kupungua huku wengine wakidai uzee umemwingia, kilichowaudhi sana Wanayanga ni pale timu yao iliporuhusu mabao matatu katika kipindi cha pili dhidi ya hasimu wao mkubwa Simba.

Yanga ilikuwa inaongoza mabao matatu hadi mapumziko na kuwafanya mashabiki wa Simba kuanza kupoteza fahamu kwa kipigo hicho, Yanga ilikuwa na hasira za kupokea kipigo kikubwa cha mabao 5-0 na Simba hivyo bao hizo tatu katika kipindi cha kwanza ni dhahiri ingeweza kupata matokeo mazuri zaidi katika kipindi cha pili.

Kwa mshangao mkubwa ulioacha maswali bila majibu, Simba ilisawazisha magoli yote matatu katika kipindi cha pili na kufanya matokeo yawe 3-3, kilio kikubwa kwa upande wa Yanga kilielekezwa kwa kipa wao Ally Mustapha 'Barthez' na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Nyota hao walisimamishwa na Yanga kwa madai ya kuihujumu timu yao, huo ndio ukawa mwisho wa Barthez kuonekana langoni mwa timu hiyo, Kipa huyo hajaonekana tena golini katika mechi mbalimbaliza ligi pamoja na za kirafiki.

Matatizo katika idara ya ulinzi ndani ya Yanga ulizidi kuonekana, mechi nyingine iliyowakera zaidi Wanayanga ni ile ya kirafiki dhidi ya Simba iliyofahamika kama Nani Mtani Jembe, kipute hicho kilifanyika uwanja wa Taifa ambapo Yanga ilichabangwa mabao 3-1, kipigo hicho kilizidi kupeleka majonzi hasa wakiwa na kumbukumbu ya sare ya maajabu ya 3-3 na Simba.

Uongozi wa Yanga safari hii ulimshutumu kiungo wake Athuman Idd 'Chuji' na kutangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana, Chuji aliomba radhi na hatimaye akasamehewa, aidha shutuma nyingine zilielekezwa kwa Cannavaro na benchi zima la ufundi.

Uongozi huo uliwafuta kazi kocha mkuu Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake Fred Minziro, kocha wa makipa Razzack Ssiwa na daktari Nassoro Matuzya.

Kutimuliwa kwa wasimamizi hao katika benchi la ufundi kulisababishwa na kipigo hicho cha mabao 3-1 toka kwa mtani wake wa jadi Simba, bado safu ya ulinzi ya Yanga ilionekana si lolote.

Ukuta wa Yanga ulikuwa chini yake Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, David Luhende na kiungo mkabaji Athuman Idd 'Chuji', mashabiki wa Yanga nao walipeleka shutuma zao kwa kipa wao Juma Kaseja ambaye aliruhusu magoli ya kizembe.

Yanga iliajili makocha wapya ambapo Mholanzi mwingine Hans Van Pluijm alitangazwa kuwa kocha mkuu, huku aliyekuwa kocha wa Ruvu Shooting Boniface Mkwassa alitangazwa kuwa msaidizi wake, Juma Pondamali alitangazwa kuwa kocha wa makipa wakati daktari ni Juma Sufiani.

Yanga ilikwenda kuweka kambi nchini Uturuki na ilitumia ziara hiyo kucheza mechi za kirafiki na iliporejea ilishuka dimbani uwanja wa Taifa kucheza na mechi ya ligi kuu mzunguko wa pili na Ashanti United.

Yanga ilianza vema ligi hiyo baada ya kuilaza Ashanti United mabao 2-1 kisha kutoka sare na Coastal Union ya Tanga 0-0kabla haijavunja rekodi ya Mbeya City kwa kuifunga bao 1-0, Mbeya City timu iliyopanda daraja msimu huu ilikuwa haijawahi kufungwa na timu yoyote ile.

Lakini katika mechi hizo, kocha mkuu wa Yanga Hans Van Pluijm aligundua mapungufu katika idaya ya ulinzi, Pluijm alimuondoa David Luhende ambaye alikuwa akicheza nambari tatu na kumuhamishia kiungo mshambuliaji.

Kitendo cha kumtoa nyuma Luhende kimeonekana kuimarisha zaidi ulinzi na kuipa nguvu safu ya ushambuliaji, kwa sasa Oscar Joshua anaimudu vema namba tatu ambapo ushirikiano wake na Cannavaro, Yondani, Twite au Juma Abdul umeifanya ngome yao kuruhusu bao moja katika mechi nne walizocheza.

Luhende alipokuwa akicheza nyuma aliigharimu timu hiyo na kusababisha kufungwa, ikumbukwe katika mechi zake mbili ilizokutana na Simba, Luhende aligeuzwa uchochoro na mawinga wa Simba.

Hata kipigo cha mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Luhende alishindwa kumkaba Ramadhani Singano 'Messi' na kumpa umaarufu wa bure, Messi kwa sasa ndiye gumzo ndani ya kikosi cha Simba na kuonekana kuwafunika wenzake.

Tangia alipoahamishwa winga ya kushambulia ameisaidia timu yake kung'ara, katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ashanti kazi kubwa ilifanywa na yeye na alifanikiwa kufunga goli moja kati ya mawili, ushindi dhidi ya Mbeya City kasi yake na Simon Msuva, Mrisho Ngassa iliwachosha mabeki wa Mbeya City na kuruhusu bao hilo.

Luhende amekuwa katika kiwango cha juu na kuanza kuumiza akili za mabeki wa timu pinzani, uchezaji wake unafanana na wa Simon Msuva na Mrisho Ngassa hivyo unaonekana kuinufaisha zaidi Yanga.

Yanga sasa inao viungo wa kukimbiza watatu ambao watawafanya washambuliaji wao Hamisi Kiiza na Didier Kavumbagu 'Uturuki' kucheka na nyavu, ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro umeonekana kuishitua Al Ahly ya Misri ambayo itacheza na Yanga katika raudni ya kwanza endapo itafanikiwa kuitoa Komorozine.

Bila shaka Yanga imelamba dume kwa Luhende ambaye sasa amegeuka lulu,Luhende aliyezwaliwa mwaka 1989 alianza kung'ara kwenye soka la ushindani akiwa na Kagera Sugar, aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa ya Vijana ambapo Yanga wakavutiwa naye na kumnasa.

Juhudi zake zilimwezesha kuitwa kwenye timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars inayonolewa na Mdenmark Kim Poulsen, lakini Poulsen amekuwa akimtumia Luhende kama mlinzi wa pembeni, je anamfuatilia vema sasa hivi ambapo anacheza kwa ustadi kiungo mshambuliaji? Tusubiri kisha tuone.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Beno Ngassa mdogo wa Mrisho Ngassa anayekipiga Tanzania Prisons