LIGI KUU BARA KIVUMBI LEO, YANGA VS ASHANTI, MTIBWA, AZAM HAPATOSHI CHAMANZI.

Baada ya kuwa katika mapumziko ya takribani miezi mitatu, Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo inaingia katika mzunguko wa pili wa lala salama, ambapo nyasi za viwanja vinne zitahitaji maji ili kuzima moto wa timu nane zitakazoshuka dimbani kukwaana.

Viwanja vitakavyowaka moto leo ni Uwanja wa Taifa na Azam Complex vya jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Mkwakwani,Tanga na Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Kwenye Uwanja wa Taifa, vinara na Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga watakabiliana na Ashanti United, wakati Azam wataikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa JKT Oljoro itakayopimana nayo ubavu kwenye Uwanja wa Mkwakwani.


Kagera Sugar wenyewe watatoana jasho na Mbeya City katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Yanga yenye pointi 28, watazindua kampeni zake za mzunguko wa pili wakiwa na mwonekano mpya katika benchi la ufundi ambalo kwa mara ya kwanza litaongozwa na kocha mpya wa timu hiyo, Mdachi Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake Charles Mkwassa.

Lakini muhimu zaidi, Yanga itaingia uwanjani huku ikibeba kumbukumbu nzuri ya matokeo ya ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Ashanti katika pambano la mzunguko wa kwanza.

Hata hivyo, hiyo haiwezi kuwa silaha tosha ya kuishinda Ashanti iliyoko nafasi ya 11, kwani hivi sasa imemwajiri kocha Abdallah Kibadeni ‘King’.

Pluijm akizungumzia maandalizi ya timu yake alisema, “Nina muda mfupi tangu nimekabidhiwa hii timu, lakini ninaweza kusema wachezaji wangu wameelewa mafunzo niliyowapa, naamini tutakuwa na mwenendo mzuri.”

Naye Kibadeni alisema,”Nina timu yenye wachezaji wenye uzoefu ambao wapo tayari kupambana, jambo zuri ni kwamba mpira unachezwa sehemu ya wazi.”

Kwa upande wake kocha wa Azam, Mcameroon Marius Omog ambaye kikosi chake kinakamata nafasi ya pili kikiwa na pointi 27 na leo kinaumana na Mtibwa alisema,”Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yalinisaidia kuwajua vizuri wachezaji wangu, nina kikosi cha kuwania ubingwa.”

Lakini mpinzani wake, Mecky Mexime ambaye ni kocha wa Mtibwa Sugar amejinadi kuwa amekipika vizuri kikosi chake akilenga kuhakikisha anavuna pointi zote tatu bila kujali anacheza na nani.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA