MAGOLI YALIYOSABABISHA VIFO VYA MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA HAYA HAPA............

Goli la pili la Yanga lililofungwa na mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza limedaiwa kusababisha kifo cha shabiki wa Simba Ramadhani Mbande, mkazi wa mtaa wa Matokeo kata ya Mabibo, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mapema jana kulienea taarifa kuwa mmoja wa mashabiki wa Simba (Mbande) alipoteza maisha wakati kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha Mholanzi Ernie Brandts kilipokuwa kikikifunga mabao mfululizo kikosi cha Simba kinachonolewa na kocha mzawa Abdallah Kibadeni 'King' katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyomazika kwa sare ya 3-3 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.


Mtandao huu ulitinga Mabibo jana mchana na kuzungumza na uongozi wa mtaa wa Matokeo na familia ya marehemu Mbande ambao walieleza kwa kina kuhusu kifo hicho.

Mjumbe wa Shina Nambari 9 la Mtaa wa Matokeo, ambako marehemu alikuwa akiishi na familia yake, Abdul Muganyizi alisema kuwa baada ya Kiiza kuifungia Yanga goli la pili, marehemu alipandwa na presha na kuishiwa nguvu akiwa amekaa kwenye kochi ndani ya nyumba yake akifuatilia mchezo huo ulioingiza Sh. milioni 500.727 zilizotokana na viingilio vya washabiki 57,422 waliokata tiketi halali kuushuhudia.

"Mimi nilikuwa kwenye baa pale jirani nikiangalia kupitia TV mchezo dhidi ya watani wetu Simba, tulipofungwa goli la kwanza huku timu yetu (Yanga) ikionekana kuzidiwa, nikaamua kukimbia kurudi nyumbani maana nami huwa na presha.

Vijana wa Simba hapa mtaani wakawa wananizomea. Kabla sijafika hata nyumbani kwangu nikapata taarifa kwamba jirani yangu Mbande amepatwa na matatizo," alisema Muganyizi.

"Nilipofika nyumbani kwake nilielezwa na mtoto wake mkubwa ambaye walikuwa wakiangalia naye mpira kuwa baba yake alipandwa na presha baada ya Simba kufungwa goli la pili.

Kabla ya hapo alikuwa akiingia ndani na kutoka kusaidia majirani ambao walikuwa wakisukumana kuchota maji kwenye bomba lake hapo nyumbani, si unajua shida ya maji hapa Dar es Salaam. Baada ya kuishia nguvu, familia yake kwa kusaidiana na majirani walimkimbiza hospitali lakini tayari alikuwa ameshatangulia mbele ya haki.

"Alikuwa na mke, watoto na wajukuu na walihamia hapa (Mabibo) baada ya serikali kubomoa nyumba za Magomeni (Dar es Salaam) ambako alikuwa akiishi na familia yake. Nililazimika kufika nyumbani kwake nikiwa kama mjumbe na jirani baada ya kupata taarifa hizo, nikatafuta sheikh na kuwatuma vijana wa mtaa wetu kushughulikia masuala ya msiba. Leo (jana) asubuhi ndugu zake wamesafirisha mwili kwenda Morogoro kwa ajili ya maziko," alisema zaidi Muganyizi.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu walisema kifo cha marehemu kilitokana na 'mipango ya Mungu' na hakina uhusiano wa moja kwa moja na mchezo wa watani wa jadi uliochezeshwa kwa ustadi mkubwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Israel Nkongo.

"Sisi tunaamini siku za baba mdogo (Mbande) zilikuwa zimefika kwa sababu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya presha kwa muda mrefu. Watu wamekihusisha kifo chake na mechi ya jana (juzi) kwa sababu tu kimetokea siku ya mechi hiyo," alisema Aisha Salum wakati akizungumza na mwandishi nyumbani kwa marehemu Mbande.

Aisha aliendelea kueleza kuwa baada ya kufika katika Hospitali ya Amana iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam, madaktari walimpima baba yake na kubaini kuwa tayari alikuwa amefariki na kwamba mwili ulihifadhiwa hospitalini hapo hadi jana asubuhi uliposafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya maziko.

Jacob Ambwene (24), ambaye baba yake Ambwene Nuaka alikuwa rafiki wa marehemu, aliliambia gazeti hili nyumbani kwa marehemu jana kuwa usafirishaji wa mwili wa marehemu ulianza majira ya saa moja asubuhi na walitegemea kuzika jana jioni mkoani Morogoro.

Katika mchezo huo wa juzi wa watani wa jadi uliokuwa ukirushwa na televisheni ya taifa (TBC1) kwa kupitia udhamini wa Azam TV walionunua haki za matangazo ya televisheni ya ligi hiyo kwa Sh. bilioni 5.6, Kiiza alifunga bao la pili la Yanga akimalizia kwa mguu wa kulia mpira wa kurushwa kama kona wa mchezaji 'kiraka' Mrwanda asili ya DRC, Mbuyu Twite dakika ya 36 ya mchezo huo ulioanza saa 10:05 alasiri.

Kiiza, ambaye aliipa Yanga goli la tatu katika dakika za majeruhi kipindi cha kwanza, alifunga goli pia katika mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo msimu uliopita ambao Yanga ilishinda 2-0 dhidi ya Simba Mei 18 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558.

Goli la kwanza la Yanga katika mchezo wa juzi iliyoshuhudia magoli manne yakifungwa na wachezaji wa kigeni, lilifungwa na winga hatari wa timu ya taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngasa katika robo saa ya mchezo huo ulioweka rekodi ya sare magoli 3-3 kila timu kumfunga, mpinzani wake mabao matatu ndani ya dakika 45 tangu timu hizo zianzishwe miaka ya 1935 na 1936.

Simba, waliowanyang'anya Yanga utawala wa mechi hiyo katika kipindi cha pili na kurejesha magoli yote matatu, walisawazisha kupitia kwa mshambuliaji waliyemsajili msimu huu akitokea klabu ya Daraja la Kwanza, Pamba ya Mwanza, Betram Mwombeki dakika ya 54, beki wa kati Mganda Joseph Owino dakika mbili kabla ya saa ya mchezo na beki mwingine wa kati Mrundi Gilbert Kaze aliyefunga kwa kichwa dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho ya refa Nkongo.

Wakati mchezo huo uliokuwa na ulinzi mkali nje na ndani ya Uwanja wa Taifa ukidaiwa kusababisha kifo cha Mbande, katika hali isiyo ya kawaida, zaidi ya washabiki 15 walianguka na kupoteza fahamu uwanjani na kuwapa kazi ya ziada watu wa msalaba mwekundu kuokoa maisha yao.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA