MAKALA: 'MATRAFIKI FEKI' TUNAO WENGI KWENYE MICHEZO

Kwa sasa kila kitu kinaendeshwa kiujanjaujanja, kama imetokea mtu kujipenyeza na kujipa ajira ya uaskari wa barabarani (traffic) kwa vitu vingine ni rahisi tu, tena  kichekesho eti alianza kazi hiyo mjini Singida.


Alijipa uhamhisho yeye mwenyewe pasipo mwajili wake mkuu, 'trafiki feki' huyo alihamia jijini Dar es salaam jiji la wajanja unaweza kuliita hivyo.

Akiwa hapa jijini trafiki huyo wa kuchonga alijitupa eneo la Kinyerezi na kuendelea  kuyapiga mabao magari yanayokiuka sheria yaani alizijua sheria zote na kuzigundua gari zinazocheza rafu barabarani.

Kwanza nampongeza kwa weledi wake huo wa kuyatambua magari yanayocheza rafu, kisha namponda kwa maamuzi yake ya kujifanya trafiki, Licha ya kujifanya trafiki wapo waliojifanya Wanajeshi ama usalama wa taifa.
Nini usalama wa usalama, Kuna watu wanajifanya mawaziri na kuwapigia watu simu na kutaka fedha, hivi karibuni kuna jamaa alijifanya yeye ndio waziri wa mambo ya ndani.

Akataka kuvuta mpunga lakini dili ikakataa, Aliyempiga kirungu ni mtoto wa mjini alishituka labda kwa sababu ya trafiki feki ambaye amejanjarusha wengi.

Jiji la Dar es Salaam lenye wajanja wengi lakini bado limeshindwa kuwabaini matapeli wa namna hii wanaojifanya trafiki feki au usalama wa taifa.


Jamaa huyo huenda aliyemchoma kwa jeshi la polisi ni mtu anayemfahamu
Kama mtu aliweza kujifanya trafiki tena kuanzia Singida hadi Dar es Salaam inaonyesha wapo watu wengi waliojichomeka kwenye idara nyeti nchini bila ya kugundulika.

Trafiki feki amekusanya zaidi ya mamilioni mpaka alipodakwa, mambo hayaendi vizuri, uchumi wetu unachezewa na wajanja wachache ambao wanatuyumbisha, licha ya tafiti mbalimbali kuonyesha kwamba uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi bado tunapata wasiwasi juu ya ukuaji wa uchumi wetu.

Uingizaji wa madawa ya kulevya umezidi kwa kasi tena mno kiasi kwamba waziri wa uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe kuingilia kwa nguvu zote,
Mwakyembe ameamua kupambana na watu wanaoingiza dawa za kulevya hapa nchini ina maana ulinzi wote uliokuwepo pale uwanja wa ndege Mwl Julius Nyerere lakini wajanja wanapitisha 'Bwimbwi'kiurahisi.

Hata mbwa wanotumika kugundua uharifu nao ‘feki’ kwa usalama wa taifa usiseme huko ndio wamejificha maofisa feki wanaodhulumu jasho la Watanzania.

Sitaki kuelezea kwa undani nisijeng’olewa kucha bure au kumwagiwa ‘tindikali’ matrafiki feki tunao wengi kwenye medani ya michezo hasa soka.

Huku kuna idadi kudwa kwa sababu soka inalipa wakishaingia tu huja na nguvu kubwa wakishafanikiwa hutokomea ghafla kama soka lipo kwenye damu kamwe huwezi kuliacha.

Wako wapi akina Jack Pemba, Alex Kajumulo na wengine wenye nguvu kama hao, walikuja na miradi mikubwa ya kuwekeza kwenye mchezo wa soka walishiriki kusaini mikataba minono lakini wakaingia mitini.

Sishangai ninapoona ahadi mabalimbali zinazotolewa na viongozi wetu wa soka hasa Simba na Yanga kukwama ni kutokana na 'trafiki feki' kuna uwezekano wengine kujulikana kupitia michezo.

Simba na Yanga zinaongozwa na 'matrafiki feki' ambao badala ya vilabu viwategemee wao, ni tofauti kidogo wao ndio wanazitegemea klabu hiko ni kichekesho kikubwa sana.

Klabu hizo zote kwa pamoja zilianzishwa na mababu zetu waliopigana kwa jasho lao miaka 77 iliyopita mababu hao waliweza kujenga misingi imara ambayo imeachwa kama urithi, majengo ni moja kati ya urithi wao ambayo yanatumika hadi sasa kama vitega uchumi.

Lakini ‘matrafiki feki’ waliopo miaka hii ya hivi karibuni wameshindwa kuziletea maendeleo zaidi, wamegeuka mahiri kwa mazungumzo Kwa kifupi Simba na Yanga hazina cha kujivunia isipokuwa kugombea wachezaji ndicho wanachoweza, utasikia mwaka huu wanamgombea Mbuyu Twite au Kelvin Yondani, mwaka mwingine Mrisho Ngassa.

Ipo siku sasa watafikia kugombea makocha au viongozi kila mmoja akidai huyo wa kwake, kwenye shirikisho letu la soka nchini TFF nako limevamiwa na ‘matrafiki feki’ sioni kama kuna mabadiliko ya kweli ni propaganda tu.
 Kupaka rangi ndiyo desturi yao ya kila siku lakini maendeleo hakuna maana ninavyoijua Tanzania! ya miaka iliyopita si hii ya sasa, Michezo yote imedorola hapa nchini wanaopewa dhamana ya kuongoza si wanamichezo wenye uchungu wa kweli, wengi wanajikita kwenye uongozi kwa malengo yao binafsi.

Ndiyo maana michezo mingine imekosa mashabiki kutokana na aina hii ya viongozi kama iliwezekana kumnasa trafiki feki aliyekuwa pale Kinyerezi basi itawezekana kuwabaini trafiki wengine waliojazana Kwenye idara nyeti ikiwemo michezo.

Wanachama wa Simba na Yanga kama mtashirikiana kwa dhati inawezekana kuwanasa wale matrafiki feki waliojipenyeza ndani ya vilabu vyenu ambao wanazitumia timu hizo kama kitega uchumi chao.

Ama sivyo umasikini kwa vilabu hivyo hautakwisha na itakuwa tatizo la timu hizo kuwa na viwanja vyake huku mkirushwa roho na habari za usajili kila kipindi chake kinaponza.

Usajili wenyewe wa kunyang’anyana wachezaji badala ya kutegemea matunda yanayotokana na uwekezaji mzuri wa vikosi vya pili vinavyotokana na akademia, kweli viongozi wa timu na shirikisho wengi wao ni matrafiki feki na ikibidi wachunguzwe ili waondolewe ama sivyo mambo hayawezi kusonga mbele.

Kila siku tunalia kuwa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu hata rais wa awamu ya pili Alhaj Ally Hassan Mwinyi aliwahi kutamka kauli hiyo, Tumechoka sasa kuburuzwa, tuonane wiki ijayo

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA