NEEMA KUBWA YAMWANGUKIA KASEJA
Kaseja amepata ‘ulaji’ huo kufuatia uongozi wa FC Lupopo kuachana na kipa wa Mtibwa Sugar, Hussein Shariff 'Cassilas' ambaye hawakukubaliana dau la uhamisho na klabu yake ya Mtibwa ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Inadaiwa kuwa Lupopo walikuwa tayari kumsajili Shariff kwa dola za Marekani 20,000, lakini baadaye Mtibwa Sugar walitaka kiasi kama hicho ili wavunje mkataba naye jambo ambalo klabu hiyo ya Kongo haikuwa tayari kwani maelezo ya awali waliyokuwa nayo ni kwamba kipa huyo alikuwa hana timu.
Habari zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam zinasema kuwa Kaseja ambaye alimaliza mkataba wa kuichezea Simba tangu Juni 30 mwaka huu atalipwa mshahara wa kila mwezi wa dola za Marekani 2,000 (Sh. milioni 3.2), kiasi ambacho inadaiwa ni kikubwa kulinganisha na mshahara aliokuwa akilipwa na klabu yake ya zamani ya ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Chanzo hicho kilifichua zaidi kwamba uongozi wa Lupopo tayari umeshafanya mazungumzo ya awali na Kaseja na hivyo kipa huyo nyota wa Stars anasubiriwa afike ili amalizane nao na kusaini mkataba.
"Hata hivyo, watu wa Lupopo wamekuwa wakimbembeleza kipa huyo ili wampe mkataba wa miaka miwili… mwenyewe Kaseja anataka asaini mkataba wa kuichezea kwa mwaka mmoja tu, ila dalili zinaonyesha watakubaliana kwavile hii ni ofa nzuri kwake (Kaseja) kwa wakati huu," kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na mtandao huu kutokea Kampala jana mchana, Kaseja alikiri kufanya mazungumzo na timu moja ya nje ya nchi na nyingine kadhaa za hapa nchini, lakini hakutaka kuzitaja timu hizo kwa maelezo kuwa bado hajahitimisha majadiliano.
Kaseja alisema vilevile kuwa baadhi ya timu zimeshindwa kufanya naye mazungumzo rasmi kwa kuhofia gharama za kumsajili, ingawa wengi wao wameonyesha kuwa kiufundi wanamhitaji sana.
"Hapa bongo zipo timu zinanisubiri nirudi ili tufanye mazungumzo na klabu moja ya nje ya nchi pia inanihitaji. Sema timu nyingi zinaniogopa kwavile wanahisi kwamba siwezi kuzikubalia au labda nitataka pesa nyingi kutokana na uzoefu wangu langoni," alisema Kaseja.
Ingawa Kaseja hakutaja timu zinazomhitaji, lakini inafahamika wazi kuwa mojawapo ni klabu ya Mbeya City ya Mbeya iliyopanda daraja na kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao. Kocha wa klabu hiyo, Juma Mwambusi, amekuwa akisema kuwa wanamuhitaji kipa huyo kwavile bado yuko katika kiwango cha juu na uzoefu wake utawasaidia sana kikosini.
Licha ya kuidakia Simba kwa takriban muongo mmoja, Kaseja pia aliwahi kuzichezea Moro United iliyokuwa Morogoro na Yanga aliyoitumikia kwa msimu mmoja.