KIMEELEWEKA, KASEJA SASA KUTUA MBEYA CITY
Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema wanamsubiri kipa wa
timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Juma Kaseja (Pichani) kumaliza majukumu yake ya Taifa
ili wafanye mazungumzo ya mwisho kwa lengo la kumtumia msimu ujao.
Mwambusi alisema bado wana imani ya kumpata kipa
huyo kwani licha ya kukosa timu mpaka sasa upo uwezekano mkubwa akawa
miongoni mwa wachezaji wake atakaowatumia katika Ligi Kuu endapo
wataafikiana.
Alisema wameshindwa kuendelea na mazungumzo na
Kaseja kutokana na sasa kuwa na majukumu katika timu ya Taifa hivyo
watamalizana naye atakaporejea kutoka Uganda.
“Bado tuna imani kubwa na Kaseja, ni miongoni mwa
wachezaji ambao uongozi unafanya juhudi za kumpata, tunaamini tutafikia
mwafaka kama mwenyewe ataridhia makubaliano yetu ili aweze kuungana na
sisi katika Ligi Kuu,” alisema Mwambusi.
Alisema kuwa kikosi chake kinaendelea vema na
maandalizi ya Ligi Kuu na kudai mashindano ya kombe la Mufindi
yameongeza hamasa zaidi kwa vijana wake na yamewaweka vizuri.
