Simba kazi bure Taifa
Kikosi cha Simba
Si tu kwamba Simba ambayo haitaweza kucheza michuano ya klabu ya Afrika mwakani haina inachopigania katika michuano hiyo karibu mwaka mmoja tangu itwae ubingwa wa Bara, bali pia ili kubaki kwenye ligi kuu, Polisi inahitaji zaidi ya miujiza.
Simba ambayo imeonekana kuathiriwa na uongozi mbovu uliopelekea kuingia katika migongano na wachezaji wake nyota, ni ya nne na hata kama itaishusha rasmi Polisi leo, itabaki katika nafasi hiyo ikiwa pointi moja nyuma ya Kagera Sugar yenye 40.
Ikiwa moja ya timu zinazoongoza kwa kutoka sare tisa nyuma ya Toto Africa na Polisi zitakazocheza ligi daraja la kwanza Taifa msimu ujao:
Simba inayotumia wachezaji yosso zaidi katika mechi zake za mwishoni ipo mbioni kushika nafasi mbovu zaidi tangu katikati ya miaka ya 1980 ilipolazimika kuifunga Yanga ili isishuke daraja.
Polisi Morogoro ni ya pili toka mkiani katika ligi ambayo zitashuka timu tatu za mwisho, ikiwa na pointi 19.
Ili kubaki kwenye daraja hilo la juu zaidi Polisi inahitaji kushinda mechi zake tatu zilizobaki ili kufikisha pointi 25 na kupunguza tofauti ya magoli, ya -10, iliyonayo.
Bahati mbaya kwa Polisi, hata hivyo, jumla hiyo imeshafikiwa na ama kupitwa na timu zote zilizo katika eneo salama la kubaki kwenye ligi kuu na zikiwa si tu na michezo iliyobaki bali pia uwiano bora wa magoli.
Mazingira hayo yanalifanya pambano kati ya Simba na Polisi kupoteza kila ladha hivyo kubaki kuwa la kukamilisha ratiba.
Ligi kuu ya Bara itaendelea Mei mosi ambapo mabingwa wapya wa Bara Yanga watakuwa wenyeji wa timu iliyoipa taji hilo ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa pia.
Sare ya Coastal Union dhidi ya Azam ndiyo iliyosababisha timu hiyo ya wauza vyakula kupoteza matumaini finyu ya kuipiku Yanga sasa ikiwa na uwezo wa kufikisha pointi 54, mbili pungufu ya ilizonazo timu hiyo ya Jangwani.
Mbali na Yanga kushuka uwanjani kwa mara ya kwanza ikiwa bingwa mpya, michezo mingine ya ligi kuu ya Bara Mei mosi ni Mtibwa Sugar itayokuwa mwenyeji wa African Lyon na JKT Ruvu itaikabili Prisons.
Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar inayowania kumaliza juu ya Simba kwa mara ya kwanza katika miaka yake tisa ya kucheza ligi kuu na Ruvu Shooting itakabili ndugu zake wa JKT Oljoro pia Mei mosi.