Yanga yapatwa pigo, Mzee Motisha aaga dunia

Familia ya Yanga imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha mwanachama wake maarufu, Mzee Said “Motisha”, aliyefariki dunia jioni ya leo.

Mzee Said Motisha alikuwa mmoja wa mashabiki na wanachama wa muda mrefu wa Yanga SC, akijulikana kwa mapenzi yake ya dhati kwa klabu hiyo. Alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakihudhuria mechi nyingi za Yanga nyumbani na ugenini, akitoa hamasa kwa wachezaji na mashabiki wenzake bila kuchoka.

Kwa miaka mingi, jina la “Motisha” lilikuwa sehemu ya utambulisho wa Yanga, huku uwepo wake ukiwa chanzo cha ari na mshikamano kwa Wananchi. Wengi walimfahamu kama shabiki wa kweli, aliyeishi na kuipenda Yanga katika nyakati za ushindi na changamoto.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na familia, maziko ya marehemu yatafanyika kesho, Ijumaa, baada ya Swala ya Alasiri.

Ibada ya mazishi itafanyika katika Msikiti wa Mwinyimkuu, kabla ya mwili wake kuzikwa katika Makaburi ya Mwinyimkuu.

Hakika mchango wake kwa familia ya Yanga utakumbukwa kwa muda mrefu. Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake, amrehemu kwa rehema zake pana, amjaalie Pepo ya Firdaus, na awape familia, ndugu, jamaa na Wanayanga wote subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Raji’un.


Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Kocha Simba anataka wachezaji wapya watano

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI