Wachambuzi na mashabiki acheni kumtoa kwenye reli Doumbia
Na Prince Hoza Matua
NI usajili muhimu uliofanywa na klabu ya Simba SC kwa ajili ya msimu huu wa 2026/2027, kamati ya usajili ya Simba ilifanya tathimini ikishirikisha benchi la ufundi.
Viongozi wa kamati ya usajili ilishirikisha makundi mengine wakiwemo viongozi wa juu wa klabu na wadhamini, miongoni mwa majina yaliyopendekezwa kusajiliwa ni mshambuliaji Ibrahim Doumbia raia wa Mali.
Wasifu wake tosha kumsajili kwani katika ligi ya nchi hiyo aliibuka kuwa mfungaji bora alifanikiwa kufunga mabao 17, ligi ya Mali ndio iliyomtoa kipa nambari moja wa Yanga Djigui Diarra ambaye pia ni miongoni mwa makipa bora kwenye ligi yeti.
Nashangaa hata ajacheza mzunguko wa kwanza tayari ameanza kuoneshewa kidole wakiashiria awamtaki, mihemko ya kishamba wanayafanya mashabiki wa Tanzania hasa wa Simba.
Kelele zinazopigwa na mashabiki wa Simba zinasapotiwa na baadhi ya wachambuzi ambao kazi yao si kulalia sehemu moja, wachambuzi wa soka hasa wa Tanzania na wao wamegeuka mashabiki.
Inanisikitisha sana mchezaji mpya hapewi muda wa kucheza na kuzoea mazingira, Ibrahim Doumbia ni mshambuliaji wa kati mwenye umbo zuri la kuitwa mshambuliaji, mrefu na ana matumizi mazuri ya kuwini mipira ya juu.
Shutuma dhidi yake ni njama za kumtoa kwenye reli, mpaka sasa Simba imecheza mechi tatu lakini lawama zilianza mechi ya pili mashabiki wakitaka mabao yake, sio siri ni tathimini za kichokozi sana zinazotaka matokeo ya papo kwa papo.
Doumbia alikuwa anakipiga AS Korofina msimu uliopita kwenye Ligi Kuu ya Mali (Mali Ligue 1 Pro), ambapo alifanya vizuri kwa kufunga mabao 17 na kutoa pasi za mabao (assist) 4.
Kwenye msimu huo, timu yake ilimaliza ikiwa na alama 31 baada ya mechi 26 (walishinda mechi 9, sare 6, na kufungwa 11). Walifunga mabao 28 na kuruhusu 33, wakiwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa wa -3.
Kiufundi, Ukiangalia takwimu, Doumbia alifunga zaidi ya nusu ya mabao yote ya timu yake (mabao 17 kati ya 28).
Hizi ni takwimu bora sana kwa mchezaji anayetoka kwenye timu ya katikati ya msimamo (mid-table team), na ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hasa kwa jinsi anavyojua kutumia mipira ya kichwa. (Kafunga mabao mengi).
Baada ya kumtazama, naona bado ana vitu vingi vya kuviendeleza (develop). Anahitaji kuboresha uwezo wake wa kukimbia na mpira mchezaji dhidi ya mchezaji (1v1 runs), pamoja na ufanisi kwenye mipira (transitions kutoka kuzuia kwenda kushambulia) hasa akiwa anakimbia na defender anayekaba tight.
Akiwa kama target man, anapaswa kujua namna ya kupokea mpira, kuulinda, au kuujaza wavuni (licha ya kufunga sana hili eneo ka struggle).
Footwork yake iko kawaida kutokana urefu wake na haipishani sana na ya Selemani Mwalimu.
Kwa kuwa ana umri wa miaka 22 tu na ana silaha ya kujua kufunga, bila shaka atafunga mabao mengi Msimbazi.
Wana kila sababu ya kufanya vizuri kwa sababu Simba SC ina “wapishi” (creative players) wengi wa kutosha.
Hivyo Sina shaka na Doumbia, ana nafasi kubwa sana ya kuwa mchezaji bora zaidi.
