Simba leo kuwakosa wachezaji wake wawili
Klabu ya Simba SC, inayofundishwa na Kocha Steve Barker, ina kibarua kizito leo Agosti 19, 2026, itakapokutana na Pamba Jiji FC katika mchezo wa NBC Premier League huku ikiwa bila huduma ya nyota wake wawili muhimu.
Mchezo huo, ambao utakuwa wa pili kwa timu zote mbili katika msimu huu, unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba saa 10:15 jioni.
Simba SC inatarajiwa kumkosa mlinda mlango wake namba moja, Mamadou Kasali, ambaye alipata maumivu katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar.
Hali hiyo inatarajiwa kumpa nafasi kipa namba mbili, Hussein Abel, kuanza katika dakika 90 za mchezo huo.Mbali na Kasali, Simba pia itamkosa beki David Kameta Duchu.
Beki huyo wa upande wa kulia alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 53 katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar baada ya kumchezea faulo beki David Luhende.
Uamuzi wa kumtoa Kameta Duchu ulifikiwa baada ya mfumo wa FVS (Football Video Support) kutumika na mwamuzi wa kati, Saad Mrope, kufanya maamuzi.
