Kiungo wa Morocco atua Manchester City

Kiungo wa kimataifa wa Morocco, Ayyoub Bouaddi, mwenye umri wa miaka 18, amekamilisha uhamisho wake kutoka Lille ya Ufaransa kwenda Manchester City, katika dili lenye thamani ya jumla ya euro milioni 100.

Manchester City imelipa euro milioni 95 kama ada ya awali, ambapo ni sawa na Shilingi bilioni 293.15 za Tanzania huku euro milioni tano zikitarajiwa kulipwa kupitia bonasi zinazoweza kufikiwa kulingana na utendaji wa mchezaji na klabu. Bouaddi amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka Etihad Stadium hadi mwaka 2031.

Uhamisho huo umemfanya Bouaddi kuwa kijana mwenye umri mdogo zaidi aliyewahi kusajiliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia ya Premier League, akivunja rekodi iliyowekwa na Leny Yoro, ambaye alihama Lille kwenda Manchester United kwa euro milioni 70 mwaka 2024.

Bouaddi anakuwa mchezaji wa pili mkubwa kusajiliwa na Manchester City katika eneo la kiungo katika dirisha hili la usajili, baada ya Elliot Anderson kujiunga na klabu hiyo akitokea Nottingham Forest.

Akizungumza baada ya kukamilisha uhamisho huo, Bouaddi amesema amefurahia kujiunga na Manchester City, akieleza kuwa amekuwa akiifuatilia klabu hiyo kwa miaka kadhaa na kuvutiwa na falsafa yake ya uchezaji.

“Manchester City kwangu ni klabu bora zaidi duniani. Ni ndoto kuwa hapa na kuweza kujiita mchezaji wa City. Nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii kwa sehemu kubwa ya maisha yangu ili kuwa mchezaji bora ninayeweza kuwa na kufikia kiwango cha juu cha mchezo.”

Ameongeza kuwa mtindo wa uchezaji wa Manchester City ni miongoni mwa sababu zilizomvutia kujiunga na klabu hiyo, akiamini kuwa ni timu yenye utamaduni wa kucheza soka lenye ubora na ushindi.



Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FIFA yatoa orodha ya vilabu bora duniani, Simba na Yanga zachuana vikali

Kocha Simba anataka wachezaji wapya watano

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI