DABI IMEHARIBU MATAMASHA
Na Prince Hoza Matua
WIKI iliyopita ilikuwa siku muhimu kwa timu zote mbili hasimu kuweza kusherehekea matamasha yake na kutambulisha vikosi vyao, ilianza Simba SC tarehe 8, Agosti ambapo iliadhimisha Simba Day.
Na kufuatiwa na Yanga SC tarehe 9 Agosti waliadhimisha Wiki ya Wananchi, kwa kifupi matamasha yote yalifana sana hasa kwenye matukio mengine mambo yalienda safi ila katika suala la mchezo kwa upande wa timu kubwa ya wanaume mambo hayakuwa mazuri.
Kwa upande wa Simba timu yao tegemezi haikufanya vizuri ingawa ilitambulisha wachezaji wake wapya, Simba ilicheza na timu ya Police FC ya Kenya na ilikubali kichapo cha bao 1-0.
Mashabiki wa timu hiyo hawakuwa na furaha baada ya kushindwa kuwaona nyota wake wapya wakionesha viwango vyao, ndivyo hivyo kwa Yanga nako walikutana na kipigo.
Yanga ilicheza na Les Aigle De Congo ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ambapo mwisho wa mchezo ilichalazwa mabao 2-1, kipigo cha Yanga nacho kimewauma mashabiki wake ambapo hawakuona viwango vya nyota wao.
Mpaka sasa si Simba wala Yanga hakuna timu iliyodiriki kuonesha viwango vya wachezaji wake kwenye matamasha hayo yalifanyika, lakini tatizo lilikuwa mechi ya dabi ambayo ilichezwa jana Jumatano.
Jana Yanga na Simba zilikutana kwenye uwanja wa New Amaan Stadium, Zanzibar, kwa kifupi makocha wa timu hizo ambao wote raia wa Afrika Kusini walishindwa kuonesha nyota zao Ili kuficha silaha.
Katika mtanange wa Jana timu zote zilifichana hivyo ilikuwa ngumu timu nyingine kujua makali ya mwenzake, Yanga ilianza na wachezaji wawili vile vile Simba ilichezesha wachezaji wawili, mashabiki wa Simba na Yanga hawakuwa na la kujivunia kupitia mchezo huo.
Timu zote hazionekana kwenye mechi za tamasha lake na kikubwa ni kuogopana, endapo Yanga wataamua kumuacha mchezaji yoyote kisa pafomansi yake haikueleweka siku ya Wiki ya Wananchi watakuwa wamemuonea.
Hiko hivyo kwa Simba ambapo timu zote zilipoteza mechi zote, matamasha ya mwaka huu nikianzia la Simba Day na Wiki ya Wananchi halikufanikiwa kwa upande wa timu.
Mashabiki wanakata tiketi za kuingilia uwanjani kushuhudia burudani lakini kubwa ni kuona mechi ya timu kubwa, mashabiki wa Simba walitaka kuona timu yao inacheza soka la kuvutia na Police FC na mwisho wa siku wanaibuka na ushindi.
Kipigo kimewaumiza sana wakiwaza kwamba timu yao haikujiandaa vyema msimu huu, Yanga nao vile vile mashabiki wake wameenda kushuhudia timu uao inatoa burudani safi na baadaye inamfunga Les Aigle De Congo.
Lakini kwa mtazamo wangu na kutumia kolamu yangu ya MIKASI nimebaini mechi ya dabi imeharibu uhondo wote na matamasha ya mwaka huu kuwa mabaya.
ALAMSIKI
